top of page
Search

Wilson Aviators Yatetemesha Dimba la Ruben FM Cup

  • heartmediak4
  • Oct 1, 2024
  • 1 min read

Na HEART MEDIA

Jumanne, 1 Oktoba 2024


TIMU ya wanaume ya Wilson Aviators inazidi kushangaza wengi baada ya kujikatia tiketi ya kushiriki fainali ya makala ya saba kuwania taji la Ruben FM Cup. Wilson Aviators FC imeibuka wembe mbele ya wapinzani wengine licha ya kwamba ndio mwanzo inashiriki kipute hicho.

Wilson Aviators ilifuzu iliponyuka Meteorite FC kwa mabao 5-4 kupitia mikwanju ya penalti

baada ya kutoka nguvu sawa mabao 2-2 ugani Vision Mukuru Kwa Njenga, Embakasi Nairobi.


Meteorite pia ilikuwa mara ya kwanza kushiriki ngarambe hiyo.

Kwenye nusu fainali ya pili, Ruben United ilicharazwa mabao 3-2 na Creative Hands. Kwenye mechi za makala ya yaliyopita ya sita, Creative Hands ilimaliza ya pili ilipopigwa na Shofco Mukuru katika fainali. ''Ninapongeza wenzangu kwa kushusha soka safi na kuhakikisha tumesonga mbele kwenye kampeni zetu,'' alisema nahodha wa Wilson Aviators, Sylvester Licham. Aliongeza kwamba wamefikia ufanisi huo kwa neema yake Mola kupitia kujituma na kujiamini bila kusahau walikabili ushindani mkali. Anadokeza kuwa kamwe hawakutarajia kama wangefuzu kushiriki fainali maana wao ni timu changa. Alitambua huduma za wenzake kwenye mechi hizo akiwamo Reyvans Kinesi, Brian Mwania, Hanington Kahi na Allan Chekaya kati ya wengine.



Kocha wa Creative Hands, Samwel Kosolo anasema wachezaji wake walifanya kazi nzuri wala hawana sababu yoyote ya kutotawazwa mabingwa wa taji la msimu huu. Kwenye robo fainali, Creative Hands ilibeba bao 1-0 mbele ya Young Warriors. Nayo Ruben United ilikomoa Vision FC kwa mabao 4-3 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1. Mshindi wa ngarambe ya mwaka huu atatuzwa Sh100,000. Timu itakayoibuka nafasi ya pili itapokea Sh70,000 kisha nafasi ya tatu na nne zitapongezwa kwa Sh40,000 na Sh20,000 mtawalia.

 
 
bottom of page