top of page
Search

Kariobangi Legends Youth, Tusker Youth Itakuwa Mechi Bab'Kubwa

  • heartmediak4
  • Nov 28, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Alhamisi 28, Novemba 2024.



KIVUMBI kikali kinatazamiwa kushuhudiwa wikendi hii kwenye mechi za Kundi C Ligi ya Taifa Daraja la Pili. Jumapili tarehe 1, Desemba Gikuni United ya kocha, Joseph Makumi na Claude Sofa itacheza na Blue Nile FC uwanjani Delmonte, Thika. Mechi Bab'kubwa itakuwa Jumamosi tarehe, 31 Novemba pale Tusker Youth itakabili Kariobangi Legends Youth ugani Ruaraka, Nairobi. ''Tunafahamu wapinzani wetu hawajapoteza mechi yoyote ambapo lazima tuwe makini zaidi tutakapowakabili,'' anasema kocha wa Tusker Youth, Charles Okere. Anaongeza kwamba wamepanga vijana wao vizuri kwa mchezo huo. Tusker Youth itashiriki mechi hiyo baada ya kutoka nguvu sawa mabao 2-2 dhidi ya Utafiti FC.



Kariobangi Legends Youth inayotiwa makali na kocha, Jemeriah Akhayo itakuwa mbioni kuwinda ushindi wa nne mfululzo. Kariobangi itaingia dimbani wiki moja baada ya kurarua Nyahururu Griffons kwa mabao 3-0. ''Kama kawaida tumejipanga kuendea ushindi wa alama tatu muhimu ili kuendelea kujiweka pazuri kwenye kampeni za msimu huu,'' anasema kocha wa Kariobangi.


Anaongeza kuwa wanafahamu wazi kuwa Tusker Youth sio timu ya kupuuza.

Kariobangi inayoshiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza, inajivunia wachana nyavu kama Bramuel Kavaya, Robbie Maangi, Paul Okumu, Victor Kinyili, Idris Amadi na Laurence Otieno kati ya wengine

Embakasi United itakuwa katika ardhi ya nyumbani kuialika Githurai All Stars (GAS) uwanjani Nyayo Estate, Embakasi Nairobi. Kwenye mechi za wiki GAS ilipigwa mabao 3-2 na Thika Sporting, Nayo Embakasi United ilitoka sare tasa mbele ya Royal Fresh.

Nyahururu Griffons imepangwa kucheza na RYSA ugani Nyahururu Stadium, mjini humo. Kocha wa Nyahururu, Joseph Mwangi anasema kuwa wameandaa kikosi hicho thabiti kulipiza kisasi baada ya pigo la wiki iliyopita. ''Bila shaka tumejipanga kiume kukabili wapinzani wetu tayari kufanya kweli kuzoa alama tatu muhimu,'' anasema kocha wa Nyahururu. Anaongeza kuwa wanafahamu wapinzani wao wamejipanga kuwalipua na kamwe hawawezi kuwapuuza.

Kwenye ratiba hiyo, South C Rangers itacheza na Tatu City, Shofco FC itaumana na Sunshine FC, Thika Sporting itakabili Utafiti FC nayo Kikuyu Township itakutanishwa na Royal Fresh.



 
 
bottom of page