Wilson Aviators, Creative Hands Patachimbika Fainali ya Ruben FM Cup
- heartmediak4
- Oct 4, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Ijumaa, 4 Septemba 2024

KIVUMBI kikali kinatazamiwa kushuhudiwa wikendi hii kwenye michuano ya kutamatisha ngarambe ya makala ya saba kuwania taji la Ruben FM Cup ugani Ruben, Kwa Ruben Embakasi, Nairobi. Kwenye mchuano wa kupigania nafasi ya tatu kitengo cha wanaume, utakaochezwa Jumamosi hii tarehe 5, Septemba 2024, Ruben United itashuka dimbani kukwaruzana na Meteorite FC.
''Bila shaka tulikubali yaishe ingawa hatukutarajia kukosa tiketi ya fainali licha ya kwamba ndio mwanzo tunashiriki shindano hili,'' anasema kocha wa Meteorite, Catherine Muoka. Anaongeza kuwa wamejiandaa kiume kukabili wapinzani wao wanakolenga kuwafinya na kumaliza tatu bora.Meteorite inajivunia huduma za wachana nyavu kama Philip Omasaja na Sylvester Patrick kati ya wengine.

Fainali ya kipute hicho itachezwa Jumapili hii tarehe 6, Septemba 2024 ambapo Wilson Aviators itakwaruzana na Creative Hands ya kocha, Samwel Kisolo iliyomaliza nafasi ya pili kwenye makala yaliyopita. ''Tumejiandaa imara kukabili wapinzani wetu lakini tunafahamu haitakuwa mteremko,'' anasema nahodha wa Wilson, Sylvester Lichama. Anaongeza kuwa wapinzani wao wanajipiga kifua maana walimaliza nafasi ya pili kwenye kampeni za makala ya mwaka uliyopita. Anadokeza kuwa wanashukuru Mungu kwa ufanisi huo maana wengi walikuwa wakiwazingua na kuwapuuza kuwa hawatafuzu kwa fainali. Wilson Aviators ambayo ndio mwanzo kushiriki kipute hicho itagemea huduma za wachezaji kama Sylvester Lichama, Reyvans Kinesi, Hanington Kahi, Allan Chekaya na Brian Mwania.
Kwenye nusu fainali Wilson Aviators iliangusha Meteorite FC kwa mabao 5-4 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa mabao 2-2. Nao wanasoka wa Creative Hands walinyamazisha Ruben United kwa mabao 3-2.

''Zitakuwa mechi gumu hasa baada ya timu zilizofuzu kwa fainali kuonyesha soka ya kuvutia kwenye michuano iliyopita,'' anasema mshirikishi wa kipute hicho, Odhis Odhat. Anaongeza kuwa waliandaa shindano la mwaka huu kuhamasisha vijana kuhusu masuala ya afya ya akili na athari za matumizi ya dawa za kulevya. Vile vile kupigana dhidi ya dhuluma za kimapenzi miongoni mwa wanawake katika mitaa ya mabanda.
Mshindi wa ngarambe ya mwaka huu atatuzwa Sh100,000. Timu itakayoibuka nafasi ya pili itapokea Sh70,000 kisha nafasi ya tatu na nne zitapongezwa kwa Sh40,000 na Sh20,000 mtawalia. Shindano la mwaka huu nilijumuisha jumla ya timu 32.


