Watch and Learn FC Yatwaa Taji la The Rissa Tournament
- heartmediak4
- Sep 10, 2024
- 1 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 10 Septemba 2024

TIMU ya Watch and Learn FC imetawazwa mabingwa wa taji la The Rissa Football Tournament kwenye mechi zilizofanyika Jumamosi tarehe 8, Septemba 2024 ugani Nairobi Sailing Club, Lang'ata Nairobi. Ngarambe hiyo iliandaliwa pia kufadhiliwa na kampuni ya simu ya Safaricom ambapo mabingwa walitia kibindoni Sh50,000 huku nafasi ya pili na tatu wakipongezwa kwa Sh25,000 na Sh15,000 mtawalia.

Watch and Learn ya kocha, Abdi Naja ilinasa ubingwa huo ilipoangusha Villaroma FC kwa mabao 5-1 katika fainali. Kwenye nusu fainali vijana hao walizoa ushindi wa magoli 4-2 mbele ya Tabiban FC. ''Bila shaka tunapongeza vijana wetu kwa kushusha soka safi na kuhakikisha wamelemea wapinzani wote ili kutwaa taji hilo,'' anasema kocha huyo. Anaongeza kuwa ufanisi wa vijana hao umewatia motisha kukaza buti zaidi kwenye mashindano tofauti hapa nchini kwa kuzingatia pia wamepania kuanza kushiriki ligi ambazo huandaliwa na shirikisho la Soka la Kenya (FKF) msimu mpya.
Anadokeza kuwa haikuwa mteremko kuibuka mabingwa wa kinyang'anyiro hicho kilichojumuisha jumla ya timu 20 kutoka maeneo tofauti katika Kaunti ya Nairobi. Watch and Learn ni kati ya timu 32 zinazoshiriki michuano ya makala ya 47 kuwania taji la Koth Biro.
Orodha ya timu zilizoshiriki ngarambe hiyo inajumuisha: Vaad FC, Santos FC, Albakar FC, Silicon, Real Madrid, Taliban, Bison, Fantasy, Kuludeng, Shilson, Al Hudda, Mid Valley, Belgo FC, Sharks, Villaroma, Predators, Wakardinals, Saints na Unknown FC


