Watch and Learn FC Tayari Kushiriki Nusu Fainali za Gozi la Koth Biro
- heartmediak4
- Nov 19, 2024
- 1 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne 19, Novemba 2024
KOCHA wa Watch and Learn FC, Abdimajid 'Naja' Mumin amejipiga kifua kwamba wamo tayari kwa nusu fainali za makala ya 47 kuwania taji la Koth Biro. Watch and Learn ilijikatia tikiti ya nusu fainali iliporarua Kayole Select FC kwa mabao 3-1 kwenye robo fainali iliyopigiwa uwanja wa Umeme Ziwani, Nairobi.

Watch and Learn FC ilipata ushindi huo kupitia juhudi zake Ahmed Abdi, Douglas Nyaosi na Morris Oduor. Kayole Select FC ilipata bao la kuvutia machozi kupitia juhudi zake Aliwa Malenya.''Katika mpango mzima tuna furaha tele kwa kunasa tikiti ya nusu fainali,'' anasema kocha wa Watch and Learn. Anangeza kuwa wamepania kupambana mwanzo mwisho kwenye nusu fainali wakipigania tikiti ya fainali.
Anadokeza kuwa anaamini wanatosha mboga kulipua wapinzani wao.
Kwenye robo fainali zingine, Eric Ayako alipiga kombora moja na kubeba Mbuta FC kunyuka Kamkunji FC bao 1-0. Nayo Mathare Commban ilishinda waliokuwa mabingwa watetezi kwa mabao 2-1 huku Kiambiu Warriors ikibeba ushindi wa mabao 3-1 mbele ya Kariadudu FC.

Kwenye mechi za raundi ya 16 bora, Watch and Learn FC ilibamiza Kahliweed FC kwa mabao 3-0, Kayole Select FC ilizoa ushindi wa mezani dhidi ya Ruaraka All Stars. Nayo Mbuta FC ilinyamazisha Leads United kwa mabao 2-1 huku Black Mamba ikidungwa bao 1-0 na Kamkunji FC.
Watch and Learn FC inajivunia kutwaa taji la The Rissa Football Tournament kwenye mechi zilizofanyika Jumamosi tarehe 8, Septemba 2024 ugani Nairobi Sailing Club, Lang'ata Nairobi. Katika fainali Watch and Learn iliangusha Villaroma FC kwa mabao 5-1 baada ya kuzoa magoli 4-2 mbele ya Tabiban FC kwenye nusu fainali.


