top of page
Search

Watch and Learn FC, Mbuta FC Hizooo Nusu Fainali Koth Biro

  • heartmediak4
  • Nov 15, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 15 Novemba 2024



TIMU ya Watch and Learn FC imeadhibu Kayole Select FC kwa mabao 3-1 kwenye robo fainali za makala ya 47 kuwania taji la Kotb Biro zilizochezwa Alhamisi (tarehe 14 Novemba 2024) ugani Umeme Ziwani, Nairobi. Naye Eric Ayako alipiga kombora moja na kubeba Mbuta FC kunyuka Kamkunji FC bao 1-0 na kutwaa tikiti ya nusu fainali. Watch and Learn FC chini ya kocha, Abdimajid 'Naja' Mumin ilishuka dimbani kwa lengo moja kurarua wapinzani wao na kusonga mbele. Watch and Learn FC ilijituma kisabuni na kutangulia kufunga mabao hayo.


Ahmed Abdi alifunga goli la kwanza, Douglas Nyaosi alitupia kimiani bao la pili huku Morris Oduor akifunga goli la tatu. Kayole Select FC ilipata bao la kuvutia machozi kupitia juhudi zake Aliwa Malenya. ''Katika mpango mzima tuna furaha tele kwa kunasa tikiti ya nusu fainali,'' anasema kocha wa Watch and Learn.





Anaongeza kuwa wamepania kupambana mwanzo mwisho kuhakikisha wanatinga fainalini. Anadokeza kuwa ni mara ya kwanza timu ya Kisomali kufuzu kwa nane bora. Anashikilia kwamba mara nyingi timu za Kisomali hufika hatua ya 16 bora. Naye naibu wake, Bonface Omino anasema wameandaa vijana wao thabiti kukabili wapinzani wao kwenye nusu fainali. ''Tunaamini tunatosha mboga kulipua wapinzani wetu na kunasa tikiti ya fainali,'' anasema.


Naye kocha wa Mbuta, Caleb Osodo anapongeza wachana nyavu wake kwa kazi nzuri waliofanya kubandua Kamkunni FC kwenye kipute cha mwaka huu.''Wengi hawakutarajia Mbuta FC ipige hatua hasa baada ya baadhi ya wachezaji waliokosa nidhamu kwenye makala zilizopita kukuzia kutoshiriki mechi za mwaka huu,'' kocha huyo anasema. Anaongeza kawaida wamepania kuendeleza mtindo wao kushiriki kila mechi kama fainali.


Kwenye mechi za raundi ya 16 bora, Watch and Learn FC ilibamiza Kahliweed FC kwa mabao 3-0, Kayole Select FC ilizoa ushindi wa mezani dhidi ya Ruaraka All Stars. Nayo Mbuta FC ilinyamazisha Leads United kwa mabao 2-1 huku Black Mamba ikidungwa bao 1-0 na Kamkunji FC.

Watch and Learn FC inajivunia kutwaa taji la The Rissa Football Tournament kwenye mechi zilizofanyika Jumamosi tarehe 8, Septemba 2024 ugani Nairobi Sailing Club, Lang'ata Nairobi. Katika fainali Watch and Learn iliangusha Villaroma FC kwa mabao 5-1 baada ya kuzoa magoli 4-2 mbele ya Tabiban FC kwenye nusu fainali.





 
 
bottom of page