top of page
Search

Washiriki Wapya Wajitosa Robo Fainali za Ruben FM Cup

  • heartmediak4
  • Sep 16, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumatatu, 16 Septemba 2024


MECHI za raundi ya 16 bora za makala ya saba kuwania taji la Ruben FM Cup zilishuhudia ushindani mkali huku baadhi ya timu zilizodhaniwa kuwa hafifu zikitwaa tiketi ya robo fainali. Mechi hizo zilichezwa Jumamosi na Jumapili (tarehe 14 na 15 Septemba) kwenye viwanja vya Vision Mukuru kwa Njenga na Ruben Mukuru Ruben, Embakasi Nairobi.


Wilson Aviators, Young Warriors na Meteorite FC zinazoshiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza zimefanikiwa kujitosa katika robo fainali. Meteorite ya kocha, Catherine Muoka iliadhibu Corinthians kwa mabao 2-1, Wilson Aviators ilizaba Green Santos magoli 4-2 nayo Young Warriors ilibeba mabao 2-0 mbele ya Gateway FC.

Meteorite iliteremsha soka safi na kulemea wapinzani wao kupitia juhudi zake Vincent Maloba na Benjamin Maina waliofunga bao moja kila mmoja. Naye Alex Mutinda alifungia Corinthians FC bao la kufuatia machozi. ''Vijana wangu walijituma kisabuni na kuhakikisha wamefanya kweli kulingana na matarajio yetu,'' anasema Herman Thungu meneja wa Meteorite. Anaongeza kwamba sasa wanapiga hesabu ya mechi za robo fainali huku wakifahamu kamwe hazitakuwa mteremko.



Nayo Young Warriors ilionyesha hataki mzaha na kufinya wapinzani wao bila huruma ambapo ilipata ushindi huo kupitia juhudi zake Elmerda Nyatuka aliyetikisa wavu mara mbili. Allan Chakaya alifungia Wilson Aviators 'Hat trick,' huku Wale Johnson akitupia kimiani bao moja. ''Tuna furaha tele kufuzu kwa robo fainali licha ya kwamba ndio mwanzo tunashiriki ngarambe ya Ruben FM Cup,'' anasema nahodha wa Wilson Aviators, Sylvester Lichama.


Naye Ben Maingi alicheka na wavu mara moja na kubeba Vision FC kudunga Nyati FC bao 1-0. Nyati FC ni kati ya vikosi vilivyopigiwa upatu kufanya vizuri kwenye ngarambe ya mwaka huu. Nayo Creative Hands ilisonga mbele baada ya kupepeta United Kings kwa mabao 3-0 kupitia mabao ya Daniel Mutinda, Carlos Mwakio na Michael Mutuku.




Nao wanasoka wa Ruben United waliangusha NAS FC kwa magoli 3-2. Wafungaji wa Ruben United walikuwa Frank Oloo, Kennedy Sidhani na Brayan Juma. Upande wa NAS FC walikuwa Godfrey Wamaswa na Moses Githinji.

Mukuru Wazee FC ilizamisha Amusha FC kwa mabao 8-7 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kutoka sare tasa. Kamongo FC ililemea Real Warriors kwa magoli 4-2 kupitia mipigo ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1. Mshindi wa makala ya mwaka huu kitengo cha wanaume atatuzwa Sh100,000 huku bingwa wa kina dada akitia kibindoni Sh40,000.

 
 
bottom of page