top of page
Search

Warembo wa Malkia Strikers Walenga Makuu Michezo ya Olimpiki

  • heartmediak4
  • Jul 12, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 12 Julai 2024


TIMU ya voliboli ya wanawake maarufu Malkia Strikers iliondoka usiku wa kuamkia Leo (Ijumaa 12 Julai 2024) kuelekea jijini Miramas, Ufaransa kwa mazoezi ya mwisho kujiandalia kipute cha Michezo ya Olimpiki Paris 2024, Ufaransa . Olimpiki za mwaka huu zimepangwa kung'oa nanga Julai 26 hadi Agosti 11.


Malkia Strikers ya kocha, Japheth Munala itashiriki ngarambe hiyo baada ya kushiriki Challenger Cup wiki iliyopita. Kocha huyo anasema kwenye kambi hiyo watakuwa mbioni kurekebisha makosa waliyogundua kwenye mechi ya Challenger walipocheza na Puerto Rico. Malkia Strikers walizabwa seti 3-0 na Puerto Rico.




''Hatujakaa vizuri kwenye safu ya mapokezi ya mipira, difensi ya mbele pia upande mwisho wa uwanja,'' alisema kocha huyo. Aliongeza kuwa wanaamini mazoezi hayo yatawasaidia. Jijini Miramas kikosi hicho kinatazamiwa kushiriki mechi nne za kirafiki dhidi ya timu za mataifa mengine pia klabu za nchini humo.


Malkia Strikers inayoshirikisha wachezaji 13 inapigwa jeki na wana dada wawili ambao hushiriki voliboli ya kulipwa katika mataifa ya bara Ulaya.

Wawili hao ni Sharon Chepchumba ambaye huchezea PAOK aliyojiunga nayo akitokea klabu ya Aris Thessaloniki. Mwingine ni Veronica Adhiambo ambaye hupigia Tarsus Belediyespor ya Uturuki.

Kwenye Michezo ya Olimpiki Malkia Strikers imepangwa Kundi B. Kundi hilo linajumuisha: mabingwa watetezi Brazil, Polland na Japan. Kwa sasa Brazil inashikilia nafasi ya pili katika msimamo wa viwango vya mchezo huo duniani (FIVB). Polland na Japan zinashikilia nafasi ya nne na saba mtawalia.

Kikosi kamili: Agripina Kundu, Sharon Chepchumba, Loice Simiyu, Pamela Adhiambo, Veronica Adhiambo, Juliana Namutira, Leonida Kasaya, Trizah Atuka (nahodha) na naibu wake Edith Wisa. Wengine Emmaculate Nekesa, Belinda Barasa, Lorine Chebet na Esther Mutinda.

Maofisa: Ofisa wa kiufundi, Paul Bitok, makocha Japheth Munala na Josp Barasa, kocha wa kupiga tizi, Janet Wanja na Mududa Waweru(daktari).

 
 
bottom of page