top of page
Search

Voliboli: Malkia Strikers Inapambana Kiume Duniani

  • heartmediak4
  • Jul 9, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumanne, 09 Julai 2024


SHIRIKISHO la Voliboli ya Kenya (KVF) limeridhishwa na matokeo ya vipusa wa timu ya taifa maarufu Malkia Strikers kwenye kipute cha Challenger Cup kilichoandaliwa jijini Manila, Ufilipino. Kwenye ngarambe hiyo, Malkia Strikers ya kocha, Japheth Munala ilimaliza ya tano kati ya vikosi nane. Matokeo hayo yamesaidia kikosi hicho kusalia nafasi ya 20 kwenye msimamo wa viwango vya mchezo huo duniani (FIVB).




''Bila shaka kwenye shindano hilo vipusa wetu walijitume kiume licha ya kuzabwa seti 3-0 na Puerto Rico,'' anasema rais wa KVF, Charles Nyaberi. Aidha amepongeza Kamati ya Michezo ya Olimpiki ya Kenya (NOCK), Java House na Mozzarbet kwa kufadhili warembo hao. Malkia Strikers imesalia namba 20 kwa kuzoa alama 157 ilhali awali ilikuwa imezoa pointi 162.





Malkia inaongoza Afrika nayo Cameroon inakamata nafasi ya pili kwa alama 135 ilhali duniani inashikilia nafasi ya 25. Misri inayokamata nafasi ya 35 duniani kwa alama 104 inafunga tatu bora Afrika. Kwenye makala ya Challenger Cup mwaka uliyopita, Kenya ilizabwa seti 3-1 na Colombia.


Kufuatia matokeo hayo, Brazil iliyokuwa inaongoza duniani ilishuka hatua moja ambapo inashikilia nafasi ya pili kwa alama 385 nayo Italia sasa inaongoza kwa alama 398.

Kwenye mechi ya kirafiki Malkia Strikers ilizoa seti 3-0 dhidi ya klabu ya The Galeries Tower Highrisers ya Ufilipino. ''Kwenye mechi yetu na Puerto Rico niligundua wasichana wangu hawapo vizuri upande wa mapokezi na difensi ya mbele,'' alisema kocha huyo. Aliongeza lazima wajaribu kujiweka vizuri kwenye mechi zijazo za kirafiki. Alisisitiza kuwa kwenye mechi yoyote wachezaji wakishindwa kupokea mipira vizuri bila shaka huwa rahisi kupoteza. Kadhalika alidokeza kuwa ulinzi wa mbele ni muhimu zaidi maana nyakati zote wapinzani huwa wanaachia kambora makali.



Warembo hao wanaelekea nchini Ufaransa kushiriki Michezo ya Olimpiki Paris 2024. Timu hiyo itaondoka kesho Jumatano tarehe 10 Julai kuelekea jijini Miramar, Ufaransa kwa mazoezi ya mwisho. Pia wakiwa jijini humo wanatarajiwa kushiriki mechi nne za kupimana nguvu. Kwenye Michezo ya Olimpiki Malkia Strikers imepangwa Kundi B linajumuisha: mabingwa watetezi Brazil, Polland na Japan.

Malkia Strikers inayoshirikisha wachezaji 16 inapigwa jeki na wana dada wawili ambao hushiriki voliboli ya kulipwa katika mataifa ya bara Ulaya. Wao ni Sharon Chepchumba (PAOK) aliyojiunga nayo akitokea klabu ya Aris Thessaloniki. Mwingine ni Veronica Adhiambo ambaye hupigia Tarsus Belediyespor ya Uturuki.

Kikosi kamili: Agripina Kundu, Linzy Jeruto, Sharon Chepchumba, Loice Simiyu, Pamela Adhiambo, Veronica Adhiambo, Juliana Namutira, Leonida Kasaya, Trizah Atuka (nahodha) na naibu wake Edith Wisa. Wengine Jemimah Siang'u, Meldina Sande, Emmaculate Nekesa, Belinda Barasa, Lorine Chebet na Esther Mutinda.

Maofisa: Ofisa wa kiufundi, Paul Bitok, makocha Japheth Munala na Josp Barasa, kocha wa kupiga tizi, Janet Wanja na Mududa Waweru(daktari).

 
 
bottom of page