top of page
Search

Voliboli: Chemasteel Yafagia Wapinzani Wengine Kibabe

  • heartmediak4
  • Nov 19, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumanne 19, Novemba 2024




TIMU ya wanaume ya Chemasteel imefagia wapinzani wao kwenye mechi tatu za mkondo wa kwanza katika voliboli ya ligi ya daraja ya kwanza zilizochezewa ugani Nyayo Stadium, Nairobi. Mechi hizo zilichezwa Ijumaa, Jumamosi na Jumapili (tarehe 15 hadi 17 Novemba).

Nayo Assassins ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) ilitunukiwa ushindi wa mechi ikiwa ufanisi wa mezani dhidi Kenya Prisons Central iliyosepa na kukosa kufika kushiriki patashika hiyo. Hata hivyo, KU ya kocha, Vitalis Ojukwu ilijipata kwenye wakati mgumu ilipokubali kulala mara mbili mbele ya Chemasteel na Seemlaw.



Chemasteel ya kocha, Jeremiah Mukopi ilizaba KU seti 3-0(25-22, 25-19, 25-14) kisha ilizoa seti 3-2 dhidi ya Vihiga Volleyball na ushindi wa mezani mbele ya Kenya Prisons Central. ''Bila shakla tuna furaha kwa kupata mwanzo mzuri kwenye kampeni zetu za kipute tuinachoshiriki kwa mara ya kwanza,'' anasema kocha wa Seemlaw. Anaongeza kuwa wamepania kuendeleza mtindo huo kwenye mechi zijazo huku wakifukuzia kumaliza kati ya nafasi mbili za kwanza ili kupandishwa ngazi msimu ujao.

Baada ya KU kunyukwa seti 3-0 na Chemasteel iliangukia pua kwenye mechi ya pili ilipocharazwa seti 3-1 na Seemlaw. ''Mechi za mkondo wa kwanza zimenifungua pakubwa ambapo lazima tujipange vingine kwenye mechi zijazo,'' anasema kocha wa KU. Anaongeza kuwa timu za wapinzani wao zinahusisha wachezaji aliowanoa wakisoma kwenye chuo hicho. KU inajivunia huduma za wachezaji shupavu kama Ibrahim Kiprotich, Faustine Kaiser, Frank Ondego na Stephen Otieno. Anadokeza kuwa amegundua kuwa anatarajia ushindani mkali mbele ya Beast, Kenya Airforce (KAF) na Beast.

Kwenye mfululizo wa matokeo ya mechi hizo, Kenya Airforce (KAF),ilibeba ufanisi wa patashika mbili na kudondosha moja, Maafande hao walizoa seti 3-1 na 3-2 mbele ya Seemlaw na Beast mtawalia kisha walibamizwa kwa seti 3-0 na Eldoret Water.

Nao maafande wa Kenya Navy walidunga Vihiga Volleyball kwa seti 3-0 vile vile walibeba ushindi sawa na huo mbele ya Deaf Volleyball. Vihiga Volleyball ilibahatika kupata ushindi wa seti 3-0 ( 25-6, 25-11, 25-17) mbele ya Deaf Volleyball. Vihiga ya kocha, Samwel Mugata ilipata ushindi huo baada ya kutunukiwa ushindi wa mezani mbele ya Pamoja Tujijenge. Masaibu ya Pamoja Tujijenge pia yalifaidi Deaf Volleyball iliyotia ufanisi wa alama tatu kapuni ilipotuzwa ufanisi wa seti 3-0.



'Kiukweli nimesoma mambo kadhaa kwa wachezaji wangu ambapo tutakuwa tunajaribu angalau kufika mapema mahali mechi zinachezewa na kupata muda wa kupumzika,'' anasema kocha wa Vihiga. Anaongeza kuwa ushindi huo umewapa motisha zaidi tayari kupambana mwanzo mwisho kwenye mechi za zijazo. Kadhalika anadokeza kwamba wakiendelea hivyo watafanya vizuri na kupandishwa ngazi msimu ujao.

 
 
bottom of page