Vita Vya Kipute cha NERL Kuendelea Kwa Mechi 11 Jijini Nairobi
- heartmediak4
- Aug 9, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Ijumaa, 9 Agosti 2024
ITA vya kufukuzia taji la FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL) zimeratibiwa kuendelea wikendi hii kwenye viwanja tofauti Kaunti ya Nairobi. Jumamosi hii tarehe 10, Agosti Lucky Summer inayoshikilia nafasi ya pili itakuwa kiamboni kukaribisha Umoja Rhinos ugani Babadogo. Nayo Mathare North United itakabili Hakati Sportiff ugani Drive Inn.

Lucky Summer ya kocha, Dan Nguya itaingia dimbani kuwinda pointi tatu ili kuendelea kujiweka pazuri kwenye mbio za kuwania taji hilo. ''Bila shaka nyakati zote kocha huandaa vijana wake tayari kuzima wapinzani wao,'' anasema kocha wa Lucky Summer. Anaongeza kuwa ana imani vijana wake watafanya kweli kwenye patashika hiyo. Lucky Summer inategemea vijana wepesi kama Dennis Opiyo, Levis Odede, Rijkaard Otieno na Joel Arika kati ya wengine.
Naye kocha wa Mathare North United, David Onyango anaamini kikosi chake kimekaa vizuri kuzima tumaini la wapinzani wao. ''Tumegundua hakuna timu ya kudharau kwenye kampeni za muhula huu,'' anasema kocha huyo.

Nao vinara wa ngarambe hiyo, Kariobangi Legends Youth Jumapili hii tarehe 11 Agosti wataalika Gunners FC ugani Kariobangi North tayari kuifunza soka. ''Kusema ukweli tutashuka dimbani tukilenga alama tatu tukitarajia mechi baadaye ili tubebe taji mapema,'' anasema kocha wa Kariobangi, Geoffrey Wangalwa. Anaongeza kuwa kama kawaida wamepania kushusha soka la kibiashara nia kuu ikiwa kuhakikisha wamezoa pointi tatu muhimu.
Kariobangi iliyoanzishwa mwaka uliyopita inajivunia wachezaji shupavu kama Victor Kinyuli, Bramuel Kasaya, George Karani, Ian Onyango (nahodha), Tom Bonfac, Dennis Wafula, Lawrence Otieno na Prise Luvutse Kati ya wengine.
Naye kocha, Josiah Olang ataongoza Automech FC kukabili Fortune Kinderen inayoendelea vibaya maana ni kati ya vikosi vilivyo katika mduara wa kushusha ngazi. ''Tunashikilia nafasi ya tano ambapo tuna kibarua kigumu kuwapiku wapinzani wetu kwa kuzingatia zimesalia mechi chache,'' anasema kocha wa Automech. Anakiri kuwa kampeni za muhula huu zinazidi kushuhudia mtihani mgumu.

Kwenye mfululizo wa michuano ya Jumapili Babadogo United imepangwa kuchuana na Tumaini FC, Ruai United itakuwa ugenini kumenyana na Uefa Despanol FC huku Wendani All Stars wakiumana na Gor Mahia Youth.
Tena United itapepetana na Soweto All Stars, Rada Sports itachuana na Pumwani Sports United, Lula FC itakabili Santos Hotspurs nayo Mathare North Youth itakutanishwa na Utawala Youth.
Kariobangi Legends Youth inaongoza kwa kuzoa alama 94, nayo Summer inashikilia nafasi ya pili kwa kusajili pointi 77 sita mbele ya Babadogo United. Utawala Youth inafunga tatu bora kwa alama 69, sita mbele ya Automech.


