Vipusa wa Twinkle Wapiga Hatua Magongo ya Supa Ligi
- heartmediak4
- Oct 13, 2024
- 1 min read
Na HEART MEDIA
Jumapili, 13 Oktoba 2024
Na HEART MEDIA
Jumapili, 13 Oktoba 2024

TIMU ya wanawake ya mpira wa magongo ya Twinkle inahitaji kushinda mechi tatu ambazo zimesalia kusudi ijiweke pazuri kumaliza kati ya nafasi mbili bora kwenye michuano ya Supa Ligi ili kupandishwa ngazi. Hii ni baada ya kurarua Vikings kwa mabao 6-0 kwenye mechi ya kipute hicho iliyochezwa Alhamisi tarehe 10 Oktoba ugani Impala, Nairobi. Mabao hayo yalipatikana kupitia, Lilian Onyango aliyepiga 'hat trick, nao Berber Atieno (nahodha), Mary Wanjiku na Love Simiyu kila mmoja alitikisa wavu mara moja.

'Ingawa tuna mtihani mgumu nina imani tukishinda mechi zilizosalia tutwaa tiketi ya kushiriki ligi kuu muhula ujao,'' alisema kocha wa Trinkle, Fredrick Masibo. Alitoa wito kwa wachezaji wake kuwa makini zaidi kwenye mechi zijazo. Kwa jumla anapongeza kikosi chake kwa kazi nzuri kinaofanya kwenye kampeni za muhula huu. Ili kukamilisha mechi za msimu huu ambazo zitachezwa kwa mkondo mmoja Twinkle itacheza dhidi ya Daystar, NCBA Wazalendo Pearls na Swans.
Kwenye mechi nyingine, wasomi wa Jomo Kenyatta (JKUAT) walikung'uta Daystar kwa magoli 4-0. Wafungaji walikuwa Abigael Wanjiru, Tabitha Njeri, Rose Wangui na Vallary Cheruto waliocheka na wavu mara moja kila mmoja.
Katika msimamo wa ngarambe hiyo, Twinkle inaongoza kwa alama 16 sawa na NCBA Wazalendo Pearls tofauti ikiwa idadi ya mabao. Nafasi ya tatu inashikiliwa na JKUAT kwa kuzoa pointi 12, moja mbele ya GHF Rift Pirates. Nayo Kisumu Queens inafunga tano bora kwa kusajili pointi saba.



