top of page
Search

Vipusa wa Kenya Wamaliza Kibabe Kwenye Bowling ya Kombe la Afrika

  • heartmediak4
  • Sep 27, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 27 Septemba 2024


TIMU ya taifa ya wanawake ya mchezo wa Bowling ilimaliza kibabe ilipotwaa medali ya fedha kwenye shindano la Kombe la Afrika lililokamilika Alhamisi tarehe 26 Septemba 2024 jijini Orapa, Botswana. Wakati huo uo mchezaji wa kitengo cha wanaume, Chris Kimanga alitwaa medali ya dhahabu kwa kuibuka mchezaji bora zaidi kwenye kipute hicho.


Warembo hao Celestine Masila, Nancy Cheruiyot, Fridah Mwangi na Eunice Mbugua walitwaa medali hiyo kwenye mechi za wachezaji wanne kila upande. Kwa jumla vipusa wa Kenya walimaliza nafasi ya pili kwenye ngarambe hiyo.

Kimanga alinasa tuzo hilo kwa kufanya vizuri kwenye mechi zote alizoshiriki ikiwa ndio mara ya kwanza kushiriki, kuonyesha nidhamu nzuri na kuwa mchezaji mchanga kwenye ngarambe hiyo kati ya vigezo zingine. ''Bila shaka nina furaha tele kwa kuzoa dhahabu kwenye kipute hicho pia napongeza wenzangu kwa mchango wao hasa kupitia ushauri wao kuhusu mchezo wa bowling,'' Kimanga anasema. Anaongeza kwamba amepania kuendeleza mtindo huo kwenye mchezo wake.



''Napongeza wenzangu wote kwa kuonyesha mchezo mzuri na kubeba medali nyingi kuliko makala yaliyopita,'' nahodha wa timu ya wanawake, Eunice Mbugua anasema.

Awali Kenya ilikuwa imetwaa medali tatu, moja ya dhahabu kitengo cha wanaume na mbili za shaba kitengo cha wanawake. Kufuatia ufanisi huo ni wazi Kenya itashiriki mashindano ya Kombe la Dunia mwaka ujao.

Kenya ilishinda dhahabu kwa timu ya wachezaji wanne kila upande kitengo cha wanaume. Kwa wanawake ilishinda shaba kwenye mechi za wachezaji watatu kila upande pia ilinasa shaba ya pili kitengo hicho kwa wachezaji wawili kila upande.

Wakenya walizoa dhahabu kwa timu ya wachezaji wanne kila upande kitengo cha wanaume iliyojumuisha Joseph Kitosi, Anwar Hamada, Kjellan Awuor na Chris Kimanga. Midume hao walipata ufanisi huo baada ya kuzaba timu ya Afrika Kusini kwa alama 21-16. Ili kushiriki mechi ya mwisho ilifuzu ilipoadhibu Zimbabwe Kwa alama 22-17.

Kitengo cha wanawake wachezaji watatu kila upande Eunice Mbugua, Fridah Mwangi na Nancy Cheruiyot walipata shaba walipolemea Zimbabwe kwa alama 21-16. Ili kufuzu kushiriki mechi hiyo Vipusa hao wa Kenya walikung'uta Namibia kwa alama 21-12.

Shaba ya pili ilipatikana kwenye mechi za wachezaji wawili kila upande baada ya Jedidah Maina na Celestine Masila kubeba ushindi wa alama 25-08 mbele ya Zimbabwe. Kabla ya patashika hiyo wawili hao walinasa tiketi ya kuishiriki waponyamazisha Botswana kwa alama 16-12.

''Napongeza wachezaji wangu kwa kufanya kwenye makala ya mwaka huu na kufuzu kushiriki fainali za kombe la Dunia mwaka ujao,'' alisema kocha wa vikosi hivyo, Andrew Jones. Anaongeza ni bidii yao iliyofanikisha kufanya bora kuliko kwenye makala yaliyopita yaliyoandaliwa nchini Namibia.


Kwenye makala yaliyopita (2023), Kenya ilizolea medali mbili ya fedha kitengo cha wanawake kategoria ya wachezaji watatu kila upande na shaba kitengo cha wanaume kategoria ya mchezaji mmoja kila upande

Timu ya wanaume ilijumuisha: Chris Kimanga, Kjellan Awuor, Anwar Hamada, Joseph Kitosi na James Ngugi. Nao wanawake ni Eunice Mbugua, Jedidah Maina, Fridah Mwangi, Nancy Cheruiyot na Celestine Masila.

Orodha ya mataifa yaliyoshiriki kipute cha mwaka huu ilijumuisha:Kenya, Zambia, Afrika Kusini, Zimbabwe, Namibia na wenyeji Botswana.

 
 
bottom of page