top of page
Search

Vikosi Vya KU Mzigoni Voliboli ya Ligi ya Vyuo Vikuu Kanda ya NRB Kaskazini.

  • heartmediak4
  • Oct 4, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 4 Septemba 2024



KAMPENI za Voliboli ya Ligi ya Vyuo Vikuu vya Kenya (KUSF) Kanda ya Nairobi Kazkasini zimepangwa kuendelea wikendi hii, (Jumamosi tarehe 5 na Jumapili tarehe 6 Septemba 2024) kwenye uga wa Chuo Kikuu Cha Kenyatta(KU), Nairobi. Timu ya Assassins na Sparrows kitengo cha wanaume na wanawake mtawalia zote za KU zimepania kuendeleza ubabe wazo baada ya kufanya kweli wiki zilizopita. ''Tunafahamu haitakuwa mteremko lakini nia yetu itakuwa kuhakikisha tunafinya wapinzani wetu ili kuendelea kujiongezea tumaini la kutesa mwaka huu,'' anasema kocha wa KU, Vitalis Ojukwu. Anaongeza kuwa wanatumia mechi za ngarambe hiyo kujinolea fainali za vyuo vikuu Afrika Mashariki na Kati (FEAUS) zitakaoandaliwa hapa nchini mwezi Desemba mwaka huu. Kwenye ngarambe ya mwaka 2022 ya Afrika Mashariki iliyoandaliwa nchini Uganda, wanaume wa KU walimaliza nafasi ya tatu baada ya kuzima Chuo Kikuu cha Kampala kwa seti 3-2.

Kwenye mechi za wiki mbili zilizotangulia wanaume wa KU walivuna seti 3-0 mbele ya Chuo Kikuu cha Kenya College Accountancy (KCA) kisha walipiga Jomo Kenyatta (JKUAT) seti 3-1. Nao warembo walibeba ufanisi wa seti 3-0 mara mbili mbele ya St Pauls (SPU) na Taasisi ya Mama Ngina (MNUC).


Kwenye ratiba ya vikosi vya KU ya mechi za Jumapili, Wanaume na wanawake vitacheza dhidi ya wenzao wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha USIU. Kwenye ratiba ya kipute hicho Jumamosi hii vipusa wa Gretsa watakabili Kwust Kenya, Daystar Falcons itamenyana na Chuo kikuu Cha Mount Kenya(MKU) huku timu ya Taasisi ya na Mama Ngina (MNUC) ikichuana na timu ya Chuo Kikuu cha Kenya College Accountancy (KCA). Nao Wanaume wa St Paul (SPU) watakutanishwa na Jomo Kenyatta (JKUAT).

Kwenye ratiba ya Jumapili, wanaume wa MKU watapepetana na Gretsa, JKUAT wataumana na MNUC nao Daystar Falcons ikivaana na KCA. Kwa wanawake, MNUC itakabili Gretsa, KCA itaumiza nyasi dhidi ya KWUST Kenya nao wachezaji wa MKU watakutanishwa na JKUAT Valley Kats.



 
 
bottom of page