top of page
Search

Vikosi Vya Bowling Wanaume na Wanawake Vinajinolea Ngarambe ya Afrika Nchini Botswana

  • heartmediak4
  • Sep 6, 2024
  • 1 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 6 Septemba 2024.




TIMU za taifa za mcheo wa Bowling kitengo cha wanaume na wanawake zinaendelea na mazoezi tayari kushiriki shindano la Kombe la Afrika (AST) litakaloandaliwa mjini Orapa, nchini Botswana. Ngarambe hiyo itafanyika Septemba 23-27 mwaka huu. Naibu rais wa Shirikisho la Kenya Bowling (KB), Pio Munyingi anasema vikosi hivyo vinaendelea na maandalizi yake katika uwanja wa Nairobi Club. ''Tunaendelea vyema na maandalizi yetu kwani tumepania kujitahidi kiume angalau tushinde nishani kadhaa kinyume na ilivyokuwa kwenye ngarambe ya makala ya mwaka uliyopita,'' alisema. Aliongeza kuwa kiwango cha mchezo huo hapa nchini kimeanza kupiga hatua baada ya kushirikisha wachezaji chipukizi.

Naibu rais huyo anadokeza kuwa wanafahamu watakabili ushindani mkali kutoka kwa mahasimu wakuu Afrika Kusini. Kadhalika alisema Afrika Kusini imepiga hatua zaidi kuliko mataifa mengine barani Afrika. Akiongea na Heart Media alisema kuwa wanatarajia kutaja vikosi vya mwisho vya wachezaji watano kitengo cha wanaume na watano kitengo cha wanawake. Hata hivyo anasema Wizara ya Michezo ndio itatoa ripoti ya mwisho kuhusu ni wachezaji wangapi watakaosafiri kuelekea Botswana kuwakilisha Kenya.

Kwenye shindano la makala yaliyopita lililoandaliwa nchini Namibia, Kenya ilijizolea nishani mbili ya fedha kitengo cha wanawake kwa wachezaji watatu na shaba kitengo cha wanaume kwa mchezaji mmoja. Orodha ya mataifa ambayo yamethibitisha kushirik kipute cha mwaka huu inajumuisha: Kenya, Zambia, Afrika Kusini, Zimbabwe, Namibia na wenyeji Botswana.

 
 
bottom of page