Vikosi Vya Bowling Tayari Kushiriki Ngarambe ya Afrika
- heartmediak4
- Sep 16, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumatatu, 16 Septemba 2024
TIMU za taifa za mchezo wa Bowling, wanaume na wanawake tayari kushiriki kipute cha Kombe la Afrika (AST) kuwania tiketi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia mwaka ujao. Wachezaji watano kitengo cha wanaume sawa na wanawake wamekamilisha mazoezi yao katika uga wa Nairobi Club tayari kuondoka Alhamisi ijayo tarehe 19, Septemba kuelekea mjini Orapa, Botswana kwa pambano hilo.
Shindano hilo litakalojumuisha nchi sita litafanyika Septemba 23-26. ''Ni imani tutapambana kiume na wapinzani wetu maana tumekuwa tukicheza nao kwenye mashindano yaliyopita ambapo nia yetu itakuwa kufanya vizuri,'' anasema nahodha wa timu ya wanawake, Eunice Mbugua. Anaongeza lazima wamakinike zaidi kwenye ngarambe hiyo. Naye nahodha wa timu ya wanaume, James Ngugi anasema wamekamilisha mazoezi yao na anaamini timu zote zimekaa vizuri kwa kidumbwedumbwe hicho.

Kenya itakuwa mbioni kuhakikisha inamaliza kati ya nafasi mbili bora ili kutwaa tiketi ya kufuzu kushiriki ngarambe ya kombe la Dunia mwaka ujao. ''Msingi wetu lazima tupambane kwa udi na uvumba kupigania tiketi ya kushiriki shindano la ubingwa wa dunia,'' anasema kocha wa vikosi hivyo, Andrew Jones. Anashikilia kwamba lazima wajitume ili wafanye vizuri kuliko walivyofanya kwenye makala ya mwaka uliyopita nchini Zambia walikozoa medali mbili pekee.
Naye rais wa Shirikisho la mchezo huo (KB), Sophy Kihuyu anasema wachezaji hao hawana sababu ya kutofanya vizuri maana wamepiga tizi ya kutosha pia serikali imejitolea kuwashika mkono.

Kwenye shindano la makala yaliyopita (2023) lililoandaliwa nchini Namibia, Kenya ilijizolea nishani mbili ya fedha kitengo cha wanawake kategoria ya wachezaji watatu na shaba kitengo cha wanaume kategoria ya mchezaji mmoja.
Timu ya wanaume inajumuisha: Chris Kimanga, Kjellan Awuor, Anwar Hamada, Joseph Kitosi na James Ngugi. Nao wanawake ni Eunice Mbugua, Jedidah Maina, Fridah Mwangi, Nancy Cheruiyot na Celestine Masila.
Orodha ya mataifa ambayo yamethibitisha kushirik kipute cha mwaka huu inajumuisha: Kenya, Zambia, Afrika Kusini, Zimbabwe, Namibia na wenyeji Botswana.


