top of page
Search

Vidume wa Wilson Aviators, Vijike wa St Josephs Starlets Wababe Ruben FM Cup

  • heartmediak4
  • Oct 8, 2024
  • 3 min read

Na HEART MEDIA

Jumanne, 8 Oktoba 2024


TIMU ya wanaume ya Wilson Aviators na wanawake wa St Josephs Starlets zimeibuka wababe wa shindano la makala ya saba ya Ruben Cup 2024. Fainali za mwaka zilichezwa Jumapili tarehe 6, Oktoba 2024. Katika kile kilichoashiria kuwa mechi hizo hazikuwa mteremko fainali na nafasi za vitengo vyote ziliamuliwa kupitia mipigo ya matuta baada ya timu husika kutoka nguvu sawa.

Katika fainali ya wanaume, Wilson Aviators ya kocha, Elijah 'Gaucho' Mwandikwa ilizamisha Creative Hands kwa magoli 5-4 baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1. Nao vigoli wa St Josephs Starlets walibeba magoli 9-8 kupitia mikwaju ya penalti mbele ya Desert Venom baada ya kukosa kufungana.



''Tunashukuru Mola kutawazwa mabingwa wa Ruben FM Cup 2024 licha ya kwamba tulikuwa limbukeni pia ilikuwa mara ya kwanza kushiriki kipute hicho,'' anasema kocha wa Wilson Aviators. Anakiri kwamba haikuwa mteremko kutinga fainali maana wapinzani wao walishusha soka la kufa mtu.


''Napongeza wachezaji wangu kwa kujituma na kulipua wapinzani wao licha ya kwamba walikuwa wametushinda kwenye mechi za makundi,'' anasema kocha wa St Joseph's Starlets. Anashikilia kuwa mashindano kama hayo husaidia wachezaji kuendelea kujifunza mengi na kuwa fiti.


Naye kocha wa Vanom Starlets, Brian muleshe anakubali yaishe na kuridhika na ushindi wa nafasi ya pili. ''Bila shaka tunashukuru kwa kujituma na kumaliza katika nafasi ya pili tukifahamu ilikuwa mwanzo kushiriki ngarambe hiyo,'' anasema.

Nafasi ya tatu kwa wanaume iliendea Meteorite FC ilipozaba Ruben United kwa mabao 4-2 kupitia mipigo ya matuta baada ya sare tasa katika muda wa kawaida. Kitengo cha kina dada, baada ya Macmillan Queens kukosa kufungana ilimaliza ya tatu ilipobeba mabao 6-5 dhidi ya Kamongoi Starlets kupitia mikwanju ya penalti.


Kwenye nusu za wanaume, Ruben United ilizabwa mabao 3-2 na Creative Hands. Nayo Wilson Aviators ilifuzu kwa fainali ilipogaragaza Meteorite FC kwa mabao 5-4 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa mabao 2-2. Vipusa wa St Josephs Starlets wafyeka Macmillan Queens kwa mabao 2-1. Desert Venom FC ililemea Kamongo Starlets 5-4 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kutoka sare tasa katika muda wa kawaida.



Tuzo ya mfungaji bora kwa wanaume iliendelea Allan Chakaya wa Wilson Aviators aliyecheka na wavu mara nane. Kwa wanawake Patience waithera wa St Josephs Starlets aliibeba baada ya kutikisa wavu mara tisa. Nao Michael Mutuku na Lindah Rachael wa Creative Hands na Desert Venom kwa wanaume na wanawake mtawalia walituzwa wachezaji wenye nidhamu bora. Waliotwaa tuzo ya wanyakaji bora walikuwa Bruno Ingudhia wa Wilson Aviators na Judith Okumu wa St Josephs Starlets kitengo cha wanaume na wanawake mtawalia.



Shindano la mwaka huu lilitumika kuhamasisha jamii kuhusu Uongozi bora, Dhuluma za kijinsia, Haki za watoto, Afya ya akili na Vita dhidi ya dawa za kulevya.

Mkurungezi wa kituo hicho, Frank O'Shea anasema wataendelea kuandaa michuano hiyo kuwapa fursa wachezaji wa vikosi vya eneo hilo kunoa makucha yao.

Meneja wa kituo hicho, Thomas 'Odhis' Opana anashukuru timu zote zilizoshiriki ngarambe ya mwaka huu kwa kujituma na kuonyesha soka nzuri. ''Ninafahamu kila timu ilipania kupambana mwanzo mwisho na kutawazwa mabingwa lakini ni timu mbili pekee zilifanikiwa,'' anasema. Anaongeza kuwa washiriki wote wanapaswa kufahamu kwamba katika mchezo wowote kuna kushinda na kushindwa.


Bingwa wa taji hilo kwa wanaume alituzwa Sh100,000, nafasi ya pili ilitia kibindoni Sh75,000 huku namba tatu na nne zikipongezwa kwa Sh50,000 na Sh30,000 mtawalia. Kwa wanawake washindi walibeba Sh40,000, nambari mbili Sh25,000 kisha namba tatu na nne Sh15,000 na Sh10,000. Kwa tuzo za kibinafsi, mfungaji bora, mnyakaji bora, mchezaji mwenye nidhamu na kocha bora kwa wanaume na wanawake kila mmoja alipokea Sh5000.

 
 
bottom of page