Vidume wa Western Jaguars Wamekaa Pazuri Kutwa Ligi Luu ya Magongo
- heartmediak4
- Nov 12, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 12 Novemba 2024

VIDUME wa Western Jaguars wanaokuja kwa kasi wanazidi kujiweka pazuri kwa mara ya kwanza kutwaa taji la ligi kuu ya magongo. Western Jaguars ambayo hunolewa na kocha, Mike Malungu imechupa kileleni kwa kuweka pengo la alama tano baina yake na Kenya Police inayokamata nafasi ya pili.
Jaguars inayojivunia kushinda mechi saba ilizoshiriki inahitaji alama nne kutoka kwa mechi mbili zilizosalia ili kubeba taji la muhula huu. Ili kukamilisha ratiba yake, Jaguars imepangwa kukabili Sailors kisha kukutanishwa na Nairobi Simba inayokamata nafasi ya nne kwa alama 12.
Wanamagongo hao wamepiga hatua hiyo baada ya kusajili ushindi kwenye mechi za Jumapili tarehe, 10 Novemba 2024, walipozaba Gladiators ya Strathmore University kwa mabao 2-1. Strathmore ilitangulia kufunga kupitia Victor San kabla ya Emmanuel Wiswa kusawazishia Jaguars na baadaye kufunga bao la ushindi. Nayo Daikyo Heroes ilipata ushindi wa pili kati ya mechi saba ambazo imeshiriki iliporarua timu ya Chuo Kikuu cha Eldoret (UoE) kwa mabao 5-3.

''Bila shaka tunaendelea vizuri kwenye kampeni za msimu huu ambapo tunaamini tumekaa pazuri kuibuka mabingwa wapya endapo tunazidisha mtindo wetu kwenye mechi mbili zilizosalia,'' anasema kocha wa Jaguars. Anangeza kuwa kampeni za muhula huu ni tofauti kabisa na misimu iliyopita maana mechi zinachezwa kwa mkondo mmoja.
Western Jaguars yenye makazi yake katika Kaunti ya Kakamega inajivunia huduma za wachezaji hodari ikiwamo Ivan Ludiali, Emmanuel Wiswa, Willis Malesi na Oscar Kibet kati ya wengine.
Katika msimamo wa kipute hicho, Mashujaa ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha USIU-A inafunga tatu bora kwa alama 12 sawa na Nairobi Simba tofauti ikiwa idadi ya mabao. Nayo Strathmore inashikilia tano bora kwa alama kumi, moja mbele ya mabingwa watetezi, Butali Warriors baada ya kuingia dimbani mara saba na nne mtawalia.


