top of page
Search

Vidume wa Western Jaguars Ndio Mabingwa Ligi Kuu ya Magongo

  • heartmediak4
  • Nov 19, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumanne 19, Novemba 2024


TIMU ya wanaume ya Western Jaguars ndio mabingwa wa ligi kuu ya magongo msimu huu baada ya kuzoa alama nne kwenye mechi za wikendi. Jaguars ya kocha, Mike Malungu inasubiria kutawazwa wafalme wa kipute hicho kwa kumaliza kampeni zake bila kushindwa.



Kwenye mechi za wikendi, Jaguars ilikung'uta Sailors kwa mabao 3-1 kisha kulazimisha kutoka nguvu sawa mabao 3-3 dhidi ya Nairobi Simba. Nairobi Simba ilishiriki mchezo huo baada ya kuzima juhudi za Butali Warriors kujiongezea tumaini la kutetea taji hilo ilipoibamiza kwa mabao 3-1.

Kwenye mechi ya kwanza, Jaguars ilijituma kwa udi na uvumba na kubeba ufanisi huo kupitia juhudi zake Derrick Juma, Alex Taiswa na Bethuel Masambu. Naye Douglas Nyerere alifungia Sailors bao la kufutia machozi. Kwenye mechi ya pili wafungaji wa Jaguars walikuwa Derrick Juma, Allan Malit na Fred Ouma waliotikisa wavu mara moja kila mmoja. Upande Nairobi Simba walikuwa Cliff Omari, Harvir Singh na Yuwras Waluiki. ''Tuna furaha tele kuibuka mabingwa wa ligi kuu msimu huu baada ya kusaka taji hilo mara mbili bila mafanikio,'' alisema nahodha wa Jaguars, Willis Malesi. Aliongeza kuwa ufanisi wao ulichangiwa pakubwa na kujituma kwao pia kujiamini wanaweza.



Western Jaguars ambayo tayari imekamilisha mechi zake inaongoza kwa kuzoa alama 25, tisa mbele ya Kenya Police ambayo ina mechi mbili kapuni. Nayo Nairobi Simba ambayo tayari imemaliza mechi zake inafunga tatu bora kwa alama 16, nne mbele ya Mashujaa ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha USIU-A ambayo imebakisha mechi tatu.




Kitengo cha wanawake juhudi za mabingwa watetezi, Blazers kujiongezea tumaini la kuhifadhi taji hilo mapema zilipigwa breki ilipodungwa bao 1-0 na Mombasa Sports Club(MSC) lililotupiwa kimiani na Jane Ofula. Naye Mirriam Mbirwa alitikisa wavu mara moja na kubeba Scorpions ya Strathmore University kusajili bao 1-0 mbele ya Lakers.


 
 
bottom of page