top of page
Search

Timu zote 22 Kuumiza Nyasi Jumapili Hii kwenye Kampeni za NERL

  • heartmediak4
  • Aug 23, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 23 Agosti 2024.


MECHI 11 zimepangwa kupigwa Jumapili hii tarehe 25 Agosti kwenye mfululizo wa kampeni za FKF Kundi B Ligi ya Nairobi Mashariki (NERL) huku macho yote yakiwa kwa Lucky Summer FC. Timu hiyo itasafiri ugenini kukabili Mathare North Youth ugani Drive Inn Primary, Thika Road kuwinda alama tatu muhimu ili kuendelea kujiweka pazuri kumaliza kati ya nafasi mbili bora. Baada ya Kariobangi Legends Youth kubeba taji la muhula huu ni wazi kuwa washiriki wengine wanapigania kumaliza nafasi ya pili.



Kariobangi inasubiria kutuzwa taji la msimu huu ambapo tayari imefuzu kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja ya Pili muhula ujao. Kwenye mfululizo wa kampeni hizo, Kariobangi ya kocha, Geoffrey Wangalwa na Jeremiah Akhayo itakuwa nyumbani kuialika Wendani All Stars ugani Kariobangi Primary.

''Tunafahamu tuna kibarua kigumu mbele ya wapinzani wetu lakini tutapambana kwa udi na uvumba kupigania pointi tatu muhimu,'' anasema kocha wa Lucky Summer, Dan Nguya. Anaongeza kuwa ana imani wachezaji wake wanatosha mboga kuvuruga wapinzani wao na kutia kapuni alama tatu. Anakiri kuwa mechi za muhula huu zinazidi kushuhudia ushindani mkali. Lucky Summer itategemea huduma za wachana nyavu wepesi kama Dennis Opiyo, Levis Odede, Rijkaard Otieno na Joel Arika kati ya wengine. Lucky Summer inakamata nafasi ya pili katika jedwali la ngarambe ya muhula huu.


Naye kocha wa Kariobangi anasema licha ya kwamba wametwaa ubingwa huo bado wamepania kuendeleza ubabe wao na kuhakikisha hawatapoteza mechi zilizosalia. Kariobangi itashuka dimbani siku chache baada ya juzi Alhamisi tarehe 22 Agosti kutoka sare tasa dhidi ya Pumwani Sports. ''Bila shaka wapinzani wetu wasitarajie mteremko bali wajipange kukabili kikosi imara na wakiteleza watapokea kichapo mbele ya vijana wangu,'' anasema kocha wa Kariobangi. Anashikilia kuwa mechi zilizosalia wanazitumia kuendelea kunoa makali yao kwa ajili ya mechi za ligi ya juu msimu ujao. Kariobangi inategemea huduma za wachezaji hodari kama Victor Kinyuli, George Karani, Tom Bonface, Lawrence Otieno, Ian Onyango (nahodha) na Bramwel Kavaya kati ya wengine.



Kwenye mfululizo wa ratiba hiyo, Rada Sports itachuana na Tena United, Tumaini FC itavaana na Ruai United, Hakati Sportiff itamenyana na Gor Mahia Youth nayo Gunners itapepetana na Umoja Rhinos. Utawala Youth itavaana na Fortune Kinderen, Santos Hotspurs itakabili Soweto All Stars, Lula FC itaumiza nyasi dhidi ya Automech FC huku Babadogo United ikikutanishwa na Pumwani Sports

 
 
bottom of page