Timu Limbukeni Zimeendelea Kutesa Kipute cha Ruben FM Cup
- heartmediak4
- Sep 24, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 24 Septemba 2024
TIMU ya Wilson Aviators na Meteorite FC zimeendelea kushangaza wengi baada ya kila moja kujikatia tiketi za nusu fainali kwenye kampeni za makala ya saba kuwania taji la Ruben FM Cup. Timu limbukeni zimefanya vizuri kwenye mashindano ya mwaka huu kinyume na ilivyokuwa kwenye makala yaliyopita.

Kwenye robo fainali, Wilson Aviators ilikung'uta Kamongo FC mabao 4-3 kupitia mipigo ya penalti baada ya kutoka sare tasa katika muda wa kawaida. Nayo Meteorite timu ya pekee kwenye kipute hicho inayofunzwa na kocha wa kike, Catherine Muoka ilipiga Mukuru Wazee kwa mabao 5-3 kupitia penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1. ''Ninashukuru wachezaji wenzangu kwa kazi nzuri waliofanya kwenye michuano ya Ruben FM Cup tunayoshiriki kwa mara ya kwanza,'' anasema nahodha wa Wilson Aviators, Sylvester Lichama. Anaongeza kuwa wamepania kupambana hadi mechi ya mwisho. Anashikilia anaamini watafinya wapinzani wao kwenye nusu fainali na kujitosa katika fainali. Anapongeza wenzake waliosaidia timu hiyo kufanya kweli akiwamo Reyvans Kinesi, Hanington Kahi, Allan Chekaya na Brian Mwania. Kwenye mechi za raundi ya 16 bora, Wilson Aviators ilizaba Green Santos kwa magoli 2-1 nayo Kamongo FC ililemea Real Warriors kwa mabao 4-2 kupitia mipigo ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1.

Naye kocha wa Meteorite anasema anafurahi tele kuongoza vijana wake kutinga nusu za ngarambe ya mwaka huu. ''Tunafahamu nusu fainali hakuna mteremko lakini sina shaka kutaja kuwa mechi zote hakuna iliyokuwa rahisi bado ninashikilia tunaweza,'' anasema. Anaongeza kuwa kwa sasa wanapiga tizi kujiandalia mechi hiyo. Meteorite iliyoshinda mechi tatu za mchujo ilifuzu kwa robo fainali baada ya kuzoa ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Corinthians kwenye mechi za raundi ya 16-Bora. Nayo Mukuru Wazee FC ilizamisha Amusha FC kwa mabao 8-7 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kutoka sare tasa.
Kwenye robo fainali zingine, Creative Hands ilibeba bao 1-0 mbele ya Young Warriors. Nayo Ruben United ilikomoa Vision FC kwa mabao 4-3 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1, Mshindi wa kitengo cha wanaume mwaka huu atatuzwa Sh100,000. Timu itakayoibuka nafasi ya pili itapokea Sh70,000 kisha nafasi ya tatu na nne zitapongezwa kwa Sh40,000 na Sh20,000 mtawalia.



