Timu 6 za Kigeni Kushiriki Voliboli ya Kipchumba Karori International
- heartmediak4
- Nov 28, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Alhamisi 28, Novemba 2024

SHINDANO la voliboli kuwania taji la Kipchumba Karori International linatazamiwa kuleta pamoja zaidi ya timu 80 ikiwamo sita za kigeni kutoka Uganda na Rwanda. Kwa mara ya kwanza katika historia ya voliboli zawadi za shindano hilo zitagharimu jumla ya Sh3.7 milioni huku mabingwa wa kiwango cha wakomavu wakituzwa Sh500,000 kitengo cha wanaume na wanawake. Ngarambe hiyo itaandaliwa mwezi ujao, Desemba 13-15 jijini Eldoret.

Orodha ya timu za kigeni inajumuisha: Nemo Stars na Kampala Amateur Volleyball Club (KAVC) wanaume na wanawake kila moja zote kutoka Uganda. Kisha Army Patriotic of Rwanda (APR) na Police Rwanda (zote wanaume) kutoka Rwanda. ''Awali shindano hili lilikuwa linajulikana kama Amaco International lakini raundi hii tumepata mfadhili mpya ndipo tukaamua kubadilisha jina,'' mshirikishi mkuu, Paul Bitok anasema kwenye hafla iliyofanyika Weston Hotel, Nairobi Jumatano 27, Novemba 2024.
Anaongeza kuwa kama Shirikisho la Voliboli ya Kenya (KVF) wamepania kutumia shindano hilo kutambua vipaji vya wachezaji chipukizi eneo hilo maana litajumuisha timu za kujitegemea pia vikosi vya vyuo vikuu, shule za upili na shule za msingi.
Kinyang'anyiro hicho kinatazamiwa kushuhudia ushindani mkali kitengo cha wakomavu kutoka kwa timu za kigeni na vikosi ambavyo hushiriki ligi kuu nchini kitengo cha wanaume na wanawake. Kitengo cha wanaume timu za ligi kuu ambavyo vimethibitisha kushiriki ni: Mamlaka ya Bandari za Kenya(KPA), Kenya Prisons, Equity Bank na Kenya General Service Unit (GSU) kati ya zingine.

Kwa wanawake zipo KCB, Jeshi la Ulinzi(KDF), Kenya Prisons na Kenya Pipeline kati ya zingine.
Timu za kujtegemea za wanaume ambazo zimethibitisha kushiriki ni kama: Huruma, Kesses, Simat, Uasin Gishu County Assembly na Tarakwa zote za Uasin Gishu. Zingine Desert Warriors (Lodwar), Nandi Flyers (Nandi), Kuresoi North (Nakuru), EMCA, Mnagei Volleyball, Kapenguria Volleyball (Kapenguria) na Highrise Kenya (Nairobi) kati ya zingine.


