Shirikisho la Bowling Limetaja Wachezaji wa Timu za Taifa Kushiriki Kombe la Afrika
- heartmediak4
- Sep 10, 2024
- 1 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 10 Septemba 2024.

SHIRIKISHO la Kenya Bowling (KB) limetoa orodha ya mwisho ya wachezaji kumi wa timu za taifa kitengo cha wanaume na wanawake watakaosafiri nchini Botswana kushiriki shindano la Kombe la Afrika (AST) baadaye mwezi huu.
Kipute hicho kitaandaliwa Septemba 23-27 mjini Orapa.
Kaimu katibu mkuu wa KB, Sam Gakuru anasema waliwasilisha majina ya wachezaji 14 kwa Wizara ya Michezo, lakini walichunjwa wanne na kusalia kumi, watano kitengo cha wanaume sawa na wanawake. ''Ni rasmi tutapeleka wachezaji kumi kushiriki ngarambe ya Kombe la Afrika mwaka huu,'' katibu huyo anasema. Ujumbe huo utaongozwa na rais wa KB, Sophy Kihuyu. Naye kocha pia aliye meneja wa vikosi hivyo atakuwa Andrew Jones.
Timu ya wanaume inajumuisha: Chris Kimanga, Kjellan Awuor, Anwar Hamada, Joseph Kitosi na James Ngugi. Nao wanawake ni Eunice Mbugua, Jedidah Maina, Fridah Mwangi, Nancy Cheruiyot na Celestine Masila.
Naibu rais wa KB, Pio Munyingi anasema vikosi hivyo vinatazamiwa kuondoka nchini Septemba 19. ''Wachezaji hao wiki hii watashiriki mazoezi mara tatu kisha wiki ijayo watakuwa huru kupumzika kabla ya kuondoka,'' naibu rais amesema. Anaongeza kuwa ana imani wanatosha mboga kufanya vizuri kwenye kipute hicho.
Kwenye shindano la makala yaliyopita (2023) lililoandaliwa nchini Namibia, Kenya ilijizolea nishani mbili ya fedha kitengo cha wanawake kategoria ya wachezaji watatu na shaba kitengo cha wanaume kategoria ya mchezaji mmoja. Orodha ya mataifa ambayo yamethibitisha kushirik kipute cha mwaka huu inajumuisha: Kenya, Zambia, Afrika Kusini, Zimbabwe, Namibia na wenyeji Botswana.


