top of page
Search

Ruben FM Cup Yaingia Mechi za Mwisho za Mchujo

  • heartmediak4
  • Sep 6, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 6 Septemba 2024


NGARAMBE ya makala ya saba kuwania taji la Ruben FM CUP inaingia mechi za mwisho za mchujo wikendi hii ambapo patashika nane zimepangwa kuchezwa kwenye viwanja vya Vision na Ruben, Embakasi Nairobi. Meteorite FC ambayo imepangwa Kundi G, Jumapili tarehe 8, Septemba 2024 itaingia mzigoni kuchuana na AFC Leopards Embakasi Branch ugani Ruben. Kwenye Kundi hilo, Dream Team itateremka kazini kukabili Ruben United ugani Vision.


Meteorite ya kocha, Catherine Muoka ambayo inaongoza Kundi hilo kwa kuzoa alama sita baada ya kushinda mechi mbili itakuwa mbioni kuwinda ushindi wa alama tatu ili kutinga hatua ya 16 bora kibabe. ''Nimeandaa wachezaji wangu kuendeleza ubabe wao na kuonyesha tunataka ubingwa wa msimu huu,'' anasema kocha huyo. Anaongeza kuwa wanafahamu wapinzani wao wamepania kuwalipua na kuvurunga mpango wao. Meteorite inajivunia kati ya wachezaji shupavu akiwamo Philip Omasaja na Sylvester Patrick kati ya wengine.

Kwenye michuano hiyo, Kamongo FC ambayo imepangwa Kundi C itashuka dimbani kumenyana na City Foxes huku ikilenga kufanya kweli na kuzoa tiketi ya kufuzu kushiriki mechi za hatua ya 16 bora. Nayo Creative Hands iliyomaliza ya pili kwenye makala yaliyopita itakwaruzana na Rising City. ''Ninaweza kutaja kuwa mechi mbili za kwanza ndizo zilizokuwa gumu lakini hii ya mwisho tunaona kama kiasi itakuwa mteremko,'' anasema kocha wa Kamongo, Enock Mukoma. Anaongeza kuwa lazima washinde ili kusonga mbele. Hata hivyo anatoa wito kwa wachezaji wangu kutolaza damu dimbani bali wajitume kufa na kupona kuhakikisha wanabeba alama zote muhimu. Kamongo inajivunia wanasoka hodari kama Anthony Kyale, Edwin Maina, Daniel Simiyu, Joseph Wamalwa, Kelvin Mutua na James Juma.



Katika msimamo wa Kundi C, Creative Hands inaongoza kwa kuzoa alama nne sawa na Kamongo tofauti ikiwa idadi ya mabao baada ya kila moja moja kushinda mechi moja na kutoka nguvu sawa mara moja. Nafasi ya tatu inashikiliwa na Rising City kwa alama tatu nayo City Foxes inashika mkia bila alama yoyote.

Kwenye mfululizo wa michuano hiyo ugani Vision, Aviation itakabili Young Warriors, FPFK itachuana na Wilson Aviators. Shofco Mukuru iliyokuwa mabingwa watetezi ambayo tayari imeondokea mbio za taji hilo itavaana na Tala All Stars huku Mukuru Wazee ikikutanishwa na Vision FC.




Orodha ya timu ambazo tayari zimefuzu kwa mechi za hatua ya 16 bora inajumuisha: Gateway FC kwa alama saba, mbili mbele ya Green Santos Katika msimamo wa Kundi B. Kundi D, Real Warriors ilimaliza kifua mbele kwa alama tisa baada ya kushinda mechi zote tatu. United Kings ilikusanya pointi nne na kumaliza nafasi ya pili. Kundi H linashirikisha NAS na Corinthians FC kwa kuvuna pointi saba na tano mtawalia. Katika msimamo wa Kundi F, Nyati FC ilimaliza kidedea kwa alama sita, moja mbele ya Amusha FC.

 
 
bottom of page