top of page
Search

Ruben FM Cup: Wilson Aviators Yajitosa Kibabe Hatua ya 16 Bora

  • heartmediak4
  • Sep 10, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumanne, 10 Septemba 2024



WILSON Aviators FC imemaliza kibabe mchujo wa makala ya saba kuwania taji la Ruben FM Cup baada ya kurarua Free Pentecostal Fellowship in Kenya (FPFK) kwa mabao 6-2 kwenye mechi zilizochezwa Jumapili tarehe 8, Septemba 2024 ugani Vision Mukuru Kwa Njenga, Embakasi Nairobi.


Kufuatia matokeo hayo, Wilson Aviators imefuzu kwa raundi ya 16 bora bila kushindwa kwa kuzoa alama tisa ikiwa kileleni mwa Kundi A. Naye Erick Juma alitikisa wavu mara moja na kusaidia Young Warriors kufuzu kwa raundi ya 16 bora ilipozaba Aviation FC kwa bao 1-0 kwenye mechi za Kundi hilo na kumaliza ya pili kwa alama sita. Wilson Aviators ilionyesha soka safi na kupata ufanisi huo kupitia Allan Chakaya mabao manne huku Sylvester Lichama akifunga mabao mawili.


Upande wa FPFK walfungaji walikuwa Simon Peter na Mario Nyabuto. ''Ni mara ya kwanza kushiriki ngarambe ya Ruben FM Cup lakini tumefanya kazi ya kupendeza,'' anasema nahodha wa Wilson Aviators, Sylvester Lichama. Anaongeza kuwa sasa wanapiga hesabu ya mechi zijazo za raundi ya 16 bora.


Kwenye mechi za Kundi G, Meteorite FC imefuzu kwa hatua ya 16 bora licha ya kuzamishwa kwa mabao 3-2 na AFC Leopards Embakasi Branch Fans.

''Licha ya kupoteza mechi ya mwisho tumefuzu kwa hatua ya 16 bora ambapo tumepania kushiriki mechi zote kama fainali,'' kocha wa Meteorite, Catherine Muoka anasema.



Kwenye kundi hilo Dream Team imesonga mbele kwa kumaliza ya pili kwa alama nne, sawa na Ruben United baada ya kutoka sare tasa.

Kundi C, Creative Hands imeponea kubaduliwa na kusonga mbele ilipolazimisha nguvu sawa mabao 2-2 dhidi ya Rising City. Nayo Kamongo FC imefuzu kwa kuibuka ya pili ilipotoka sare tasa na City Foxes.


Timu zingine ambazo zimesonga mbele zikiwa Nyati FC kwenye mechi za Kundi F kwa kuzoa alama sita, moja mbele ya Amusha FC. Nyingine ni Gateway FC kwa alama saba, mbili mbele ya Green Santos katika Kundi B. Kundi D, Real Warriors ilimaliza kifua mbele kwa alama tisa baada ya kushinda mechi zote tatu. United Kings ilikusanya pointi nne na kumaliza nafasi ya pili. Kundi H linashirikisha NAS na Corinthians FC kwa kuvuna pointi saba na tano mtawalia. Mshindi wa makala ya mwaka huu kitengo cha wanaume atatuzwa Sh100,000 huku bingwa wa kina dada akitia kibindoni Sh40,000.

 
 
bottom of page