Ruben FM Cup Wikendi Hii: Nyati FC, Corinthians FC Kila Moja 'Ni Must Win'
- heartmediak4
- Aug 30, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Ijumaa, 30 Agosti 2024.
NYATI FC na Corinthians FC kila moja ina mtihani mgumu wikendi hii kwenye kampeni za makala ya saba kuwania taji la Ruben FM Cup. Corinthians FC ya kocha, Silas Kivasu Jumamosi hii tarehe 31, Agosti itashuka dimbani kukabili NAS FC ugani Ruben, Embakasi Nairobi. Nayo Nyati FC Jumapili hii tarehe 1 Septemba itaingia mzigoni kumenyana na Minto FC.

''Tumejipanga kiume kukabili wapinzani wetu ambapo tutakuwa mbioni kuwinda ushindi wa alama tatu ama kutoka nguvu sawa ili kujiweka pazuri kunasa tiketi ya kusonga mbele,'' anasema kocha wa Corinthians. Anaongeza kuwa wakipoteza mechi hiyo watakuwa na nafasi vinyu kabisa ya kusonga mbele. Kwenye mechi za kwanza Corinthians ilipiga Barca Veterans 2-1 kisha kutoka sare tasa na Embakasi East. Corinthians inajivunia wachezaji shupavu kama Alex Mutinda (nahodha), Brian Iwobi, Denis 'Lefty', Aron Kimanzi, John Andere na Analo Steven kati ya wengine.
Nayo Nyati FC ya kocha, Michael Wanjohi itahitaji kunyamazisha Minto FC ili kusonga mbele kushiriki mechi za hatua ya 16 bora. ''Buda tunafahamu ni 'must win match' wala hakuna chenga endapo tunahitaji kusonga mbele.'' anasema mwanzilishi wa Nyati FC, Curtis Saiti. Anaongeza kuwa wameandaa wachezaji wao tayari kutifua vumbi la kufa mtu wala hawana lingine.

Pia Minto FC kwa asilimia kubwa itakuwa inataka ushindi wa alama tatu muhimu ili kujiweka pazuri kusonga mbele. Kwenye utangulizi wa kipute hicho, Nyati FC iliangusha Deportivo Leon kwa mabao 2-0 kabla ya kuzabwa mabao 3-0 na Amusha FC. Nyati FC inategemea huduma za wachezaji bomba kama Jesse Inanga, Josephat Nyamunte, Rodgers Mbasu, Felix Onyango na Faberson Kyalo.
Kwenye mfululizo wa ratiba hiyo, United Kings itahitaji kupambana kwa udi na uvumba kuhakikisha inashinda Simba FC ili kuzoa tiketi ya kusonga mbele. United Kings inajivunia kushinda kwa mabao 5-2 dhidi ya Busec FC kisha kukubali kulala kwa bao 1-0 mbele ya Real Warriors.
Baada ya Tala All Stars kuachia alama tatu muhimu mbele ya Vision FC wiki mbili zilizopita wikendi hii imepangwa kushuka dimbani kukabili Mukuru Wazee.
Barca Veterans itaumana na Embakasi East FC, Homeboyz itaonana na Gateway FC, Deportivo Leon itatifua vumbi dhidi ya Amusha FC, Busec itapepetana na Real Warriors huku Milan FC ikikutanishwa na Green Santos.
Mshindi wa makala ya mwaka huu kitengo cha wanaume atatuzwa Sh100,000 huku bingwa wa kina dada akitia kibindoni Sh40,000. Kwa wanaume nafasi ya pili na tatu watapokea Sh70,000 na 40,000 huku nambari nne akipongezwa kwa Sh20,000. Kwa wanawake timu itakayoibuka ya pili itazoa Sh25,000 nafasi ya tatu na nne zitatuzwa Sh15,000 na Sh10,000 mtawalia. Kwa tuzo za kibinafsi, mfungaji bora, mnyakaji bora, mchezaji mwenye nidhamu na kocha bora kwa wanaume na wanawake kila mmoja atapokea Sh5, 000.


