top of page
Search

Ruben FM Cup: St Josephs Starlets Waleteni Hao Wana Desert Venom

  • heartmediak4
  • Oct 4, 2024
  • 1 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 4 Septemba 2024


KAMPENI za makala ya saba kuwania taji la Ruben FM Cup zitafikia kikomo wikendi hii. Fainali ya kina dada itashirikisha timu ambazo hazijawahi kushiriki shindano hilo baada ya Embakasi South Ladies United iliyokuwa inajivunia kubeba taji hilo mara mbili kubanduliwa kwenye mechi za mchujo. Fainali itachezwa Jumapili tarehe 6, Septemba 2024 nayo nafasi ya tatu itachezwa Jumamosi tarehe 5, Septemba 2024 ugani Ruben, Kwa Ruben Embakasi, Nairobi.

Kwenye mechi ya kuwania nafasi ya tatu, Macmillan itachuana na Kamongo Starlers. Katika St Joseph Starlets ya kocha, Kipchirchir Limo itakutanishwa na Desert Venom.

''Ninaamini vigoli wangu watafanya kweli jinsi walivyotesa kwenye mechi za mchujo hadi nusu fainali,'' anasema kocha wa St Josephs Starlets.


Anatoa wito kwa wachezaji wake kutolaza damu dimbani maana hawana lingine bali wanataka kubeba taji la msimu huu. Hata hivyo anakiri kuwa itakuwa kibarua kigumu maana wapinzani wao waliwacharaza kwenye mechi za makundi. Kocha huyo anasifia baadhi ya wachezaji wake kwa kazi nzuri waliofanya kwenye mechi zilizopita. Anataja wachezaji hao kama Sheril Atieno (nahodha), Ivy Norah, Judy Akumu, Fatuma Mohammed na Patience Waithera.

Kwenye nusu fainali, St Josephs Starlets ilinyamazisha Macmillan Queens kwa kuidunga mabao 2-1. Embakasi South Ladies United ilitolewa kwenye kipute cha mwaka huu ilipozabwa bao 1-0 na Kamongo Starlets kwenye mechi ya mwisho ya mchujo.

Kwenye nusu fainali ya pili, Desert Venom FC ililemea Kamongo Starlets kwa mabao 5-4 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kutoka sare tasa katika muda wa kawaida. Bingwa wa mwaka huu atatuzwa Sh40,000, nafasi ya pili atapokea Sh25,000, nafasi ya tatu na nne zitatuzwa Sh15,000 na Sh10,000 mtawalia.



 
 
bottom of page