Ruben FM Cup: Minto, Mukuru Wazee Zavuna, Nyati, Shofco Zikijikwaa
- heartmediak4
- Aug 20, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 20 Agosti 2024

MICHUANO ya Ruben FM Cup imeonyesha ushindani wa aina yake baada ya kipute hicho kuingia raundi ya tatu wikendi iliyopita. Kwenye matokeo ya Jumapili 18 Agosti, Nyati FC ililambishwa kichapo cha kwanza ilipolala kwa magoli 3-0 mbele ya Amusha FC, Deportivo FC ilipata pigo la pili huku Vision FC ikizoa ushindi wa mezani mbele ya Tala Allstars. Danny Obara ilitikisa wavu mara moja na kubeba Minto FC kuchapa Deportivo FC kwa bao 1-0. Mabao ya Amusha FC yalipatikana kupitia juhudi zake Lawrence Otieno aliyetikisa wavu mara mbili huku Austin Kefa akiangusha kombora moja. ''Tulijipata pabaya kwenye mchuano huo ambapo sasa ni lazima tushinde mechi iliyosalia tena kwa mabao mengi ili kujiweka pazuri kusonga mbele,'' anasema kocha mkuu wa Nyati FC, Michael Wanjohi. Hata hivyo anashikilia kuwa kupoteza mechi hiyo ni pigo kubwa kulingana na uliyokuwa mpango wao kwenye kampeni za msimu huu.

Nao mabingwa watetezi, Shofco Mukuru ya kocha, William Kilyungi ilianza kampeni zake vibaya iliponyukwa kwa mabao 3-1 na Mukuru Wazee FC. Kikosi cha Wazee Mukuru kilibeba ufanisi huo kupitia juhudi zake Julius Aseko aliyetikisa wavu mara mbili huku Simon Abuko akitupia kimiani bao moja.
Kwenye matokeo hayo, Creative Hands ililazimishwa kutoka nguvu sawa bao 1-1 na Kamongo FC. Creative Hands ilifungiwa bao hilo na Caleb Abuga huku Edwin Maina akisawazishia Kamongo FC.
Tumaini la Corinthians kufanya kweli liligonga ukuta ilipotoka sare tasa na Embakasi East FC huku Busec FC ikisajili matokeo sawa dhidi ya Simba FC.
Mshindi wa makala ya mwaka huu kitengo cha wanaume atatuzwa Sh100,000 huku bingwa wa kina dada akitia kibindoni Sh40,000. Kwa wanaume nafasi ya pili na tatu watapokea Sh70,000 na 40,000 huku nambari nne akipongezwa kwa Sh20,000. Kwa wanawake timu itakayoibuka ya pili itazoa Sh25,000 nafasi ya tatu na nne zitatuzwa Sh15,000 na Sh10,000 mtawalia. Kwa tuzo za kibinafsi, mfungaji bora, mnyakaji bora, mchezaji mwenye nidhamu na kocha bora kwa wanaume na wanawake kila mmoja atapokea Sh5000.


