Ruben FM Cup: Mechi za 16-Bora Kupigwa Wikendi hii
- heartmediak4
- Sep 13, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Ijumaa, 13 Septemba 2024
KIVUMBI kikali kinatazamiwa kushuhudiwa wikendi hii kwenye mechi za raundi ya 16 bora za makala ya saba kuwania taji la Ruben FM Cup. Nyati FC imepangwa kukabili majirani zao Vision FC kwenye mechi zitakaochezwa Jumapili tarehe 15 Septemba 2024 ugani Vision, Mukuru Kwa Njenga Embakasi, Nairobi. Nyati FC ya kocha, Michael Wanjohi itahitaji kupambana kwa udi na uvumba ili kuzima majirani zao na kutwaa tiketi ya robo fainali.

Ofisa mkuu wake, Curtis Saiti anasema itakuwa mechi gumu kwa kuzingatia majirani zao wanafahamu bayana mchezo wao maana pia hufanyia mazoezi uwanja mmoja. ''Tumeandaa vijana wetu tayari kukabili wapinzani wetu kwenye mechi ambayo lazima tushinde ili tusonge mbele,'' anasema ofisa huyo. Anaongeza kuwa wanaelewa wana kibarua kigumu lakini dakika tisini ndizo zitakaoamua nani mkali.
Kwenye safu ya difensi Nyati FC inajivunia wachezaji shupavu kama Oscar Emmanuel na Rodgers Tangasi, kiungo cha kati Felix Omeny nao washambuliaji wakiwa Elvis Omolet na Rodgers Mbasu. Nyati ilijikatia tiketi ya mechi za 16 bora baada ya kumaliza ya pili kwa alama sita nayo Amusha FC iliibuka kidedea kwa alama saba katika msimamo wa Kundi F. Katika jedwali la Kundi E, Vision ilimaliza kifua mbele kwa alama sita, mbili mbele ya Mukuru Wazee FC.

Mechi nyingine itakuwa kati ya Wilson Aviators na Green Santos ugani Ruben, Mukuru Kwa Ruben, Embakasi Nairobi. Nahodha wa Wilson Aviators, Sylvester Lishama inayoshiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza anasema wanatarajia mtihani mgumu kwa kuzingatia timu yoyote kutinga kiwango hicho inaashiria sio rahisi. ''Ninaweza kusema kuwa hakuna timu ya kupuuza kwanza mahali ngarambe hiyo imefikia ni hatua ya mauano hakuna kulaza damu dimbani.
Wilson Aviators itategemea huduma za wachezaji kama Reyvans Kinesi, Sylvester Lishama, Hanington Kahi, Allan Chakaya na Brian Mwania. Katika msimamo wa Kundi A, Wilson Aviators ilimaliza kileleni kwa alama tisa baada ya kushinda mechi zote tatu, nayo Young Warriors ilizoa alama sita na kuibuka ya pili. Green Santos iliyokuwa imepangwa Kundi B ilimaliza ya pili kwa alama tano nayo Gateway FC kwa alama saba ilikuwa ya kwanza.

Kwenye ratiba hiyo, kocha Catherine Muoka ataiongoza Meteorite FC kukabili Corinthians FC ugani Vision.. Amusha FC itamenyana na Mukuru Wazee, Gateway FC itakwaruzana na Young Warriors, Creative Hands itaivaa United Kings, Nas S itapepetana na Ruben United huku Kamongo FC ikikutanishwa na Real Warriors.


