top of page
Search

Ruben FM Cup: Kivumbi Kikali Kinanukia Huku Ikitinga Raundi ya 3

  • heartmediak4
  • Aug 23, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 23 Agosti 2024





MICHUANO ya soka kufukuzia ubingwa wa makala ya saba ya Ruben FM Cup inaingia wiki ya tatu wikendi hii (Jumamosi tarehe 24 Agosti na Jumapili tarehe 25 Agosti), ambapo mechi 12 zimepangwa kuchezwa kwenye viwanja vya Vision, Embakasi Girls na Reuben eneo la Embakasi, Nairobi. Shofco Mukuru FC ya kocha, William Kilyungi ambayo ndio mabingwa watetezi itakuwa mbioni kuwinda ushindi wa kwanza itakaposhuka dimbani kukabili Vision FC. Nayo Kamongo FC imepangwa kuvaana na Rising City.

Shofco ilianza vibaya iliponyukwa mabao 3-1 na Mukuru Wazee nayo Vision FC ilipata ushindi wa mezani baada ya wapinzani wao Tala All Stars kuingia mitini. ''Sina shaka kutaja kuwa tunatarajia mchezo mgumu hasa baada ya kupata kichapo kwenye mchuano wa kwanza,'' anasema kocha wa Shofco. Anaongeza kuwa licha ya hayo wamejipanga kushusha soka la kibiashara. Shofco inajivunia wachezaji machachari kama Thomas John, Kennedy Kibe, Jacob Kelly, Fidel Andewa na Victor Onduso.


''Tulianza vibaya kampeni zetu ambapo tutahitaji kushinda mechi hiyo ili kukaa pazuri kusonga mbele,'' anasema kocha wa Kamongo FC, Enock Mukoma. Anashikilia kuwa ana imani wachezaji wake wataonyesha mechi nzuri kwani lazima wajitahidi kiume kuhakikisha wanatinga hatua ya 16 bora. Kamongo itategemea huduma za wachezaji hodari kama Brayant Machio, Kelvin Nyandoro, Joseph Wamalwa, Maxwell Makokha na Anthony Idorot kati ya wengine..



Kwenye mechi nyingine, Creative Hands wamepangwa kumenyana na City Foxes. Creative Hands ilishuka dimbani baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 na Kamongo FC.

Wilson Aviators itapepetana na Young Warriors. Nahodha wa Wislon Aviators, Sylvester Lishama anasema kuwa wapo tayari kubeba ushindi wa alama tatu muhimu ili kujiweka pazuri kufanya kweli ikiwa ndio mwanzo kushiriki ngarambe hiyo. Kwenye utangulizi wa mechi zao Wilson Aviators ilisajili ufanisi wa mabao 2-1 dhidi ya Aviation FC.

Kwenye mfululizo wa ratiba hiyo, Green Santos itachuana na Gateway FC, Homeboyz FC itaumana na Milan FC, Milan FC itacheza mechi ya pili dhidi ya Gateway FC, huku Real Warriors ikichuana na Simba FC. Meteorite FC itaumiza nyasi na Dream, Busec itakabili United Kings, AFC Leopards Embakasi Branch itagaragazana na Ruben United huku FPFK ikikutanishwa na Aviation FC. ''Tunatarajia ushindi wa zaidi ya mabao matatu ili kujiweka pazuri kwenye mechi za mwaka huu,'' anasema kocha mkuu wa FPFK, Edwin Manwa. Anaongeza kuwa wamepania kufanya vizuri kuliko mwaka uliyopita ambapo walibanduliwa katika robo fainali. FPFK itategemea wachezaji wepesi kama Boniface Kamau ambaye ndiye mwanzilishi wa timu hiyo. Pia wapo Samuel Korogo, Bencliff Isika, Morgan Mutinda na Daniel 'Danteh' Mburukati ya wengine.

Kwenye mechi zilizotangulia Simba FC ililazimishwa kutoka sare tasa na Busec FC. Mshindi wa makala ya mwaka huu kitengo cha wanaume atatuzwa Sh100,000 huku bingwa wa kina dada akitia kibindoni Sh40,000.

 
 
bottom of page