Ruben FM Cup: Embakasi South Ladies Inahitaji Muujiza
- heartmediak4
- Sep 27, 2024
- 1 min read
Na HEART MEDIA
Ijumaa, 27 Septemba 2024

TIMU ya wanawake ya Embakasi South Ladies United Jumamosi hii tarehe 28 Septemba 2024 itahitaji kunyamazisha Kamongo Starlets ili kunasa tiketi ya nusu fainali za makala ya saba kuwania taji la Ruben FM Cup. Mechi hizo zitachezewa ugani Vision Mukuru Kwa Njenga, Embakasi Nairobi. Embakasi South ndio mabingwa watetezi wa taji hilo ambalo imeshinda mara mbili mfululizo baada ta kulipigania mara tatu.
Kocha wake, Everlyne Onyango anasema wanafahamu wana kibarua kigumu mbele ya wapinzani wao maana wanahesabiwa kama kizuizi kikuu. ''Tumejipanga kiume kukabili wapinzani wetu ambapo lazima tuwe makini zaidi tusirejelee makosa tuliyofanya wiki iliyopita tulipodondosha mechi moja mbele ya Macmillan Queens,'' anaema. Anaongeza kuwa dakika tisini uwanjani ndizo zitakaoamua nani mkali. Embakasi South imepangwa Kundi A ambapo inashikilia nafasi ya tatu kwa alama tatu sawa na Kamongo inayokamata nafasi ya pili kwa kuzoa idadi kubwa ya mabao ya ushindi.
Embakasi South ikipoteza mechi hiyo ama itoke nguvu sawa haitakuwa na lingine bali itaenda nyumbani kusubiria kipute cha mwaka ujao. Kwenye mfululIzo wa mechi hizo za mwisho za mchujo, Macmillan Queens inapigiwa chapuo kurarua Wilson Aviators na kuendelea kujiongezea tumaini la kubeba ubingwa wa mwaka huu.
Kwenye mechi za Kundi B, Desert Venom FC inayojivunia kushinda mechi mbili, itashuka dimbani kukabili Mukuru Talent nayo Mukuru Transformers itaingia mzigoni kukutanishwa na St Joseph Starlets. Bingwa wa mwaka huu atatuzwa Sh40,000, nafasi ya pili atapokea Sh25,000, nafasi ya tatu na nne zitatuzwa Sh15,000 na Sh10,000 mtawalia.


