Ruben FM Cup: Embakasi South Ladies Imeapa Kukiwacha
- heartmediak4
- Sep 21, 2024
- 1 min read
Na HEART MEDIA
Jumamosi, 21 Septemba 2024

KLABU ya wanawake ya Embakasi South Ladies United imeapa kupambana mwanzo mwisho itakapokabili Macmillan Queens kwenye utangulizi wa mechi za kitengo hicho za makala ya saba kuwania taji la Ruben FM Cup wikendi hii. Timu hizo zitakutanishwa Jumamosi hii tarehe 21 Septemba 2024 ugani Embakasi Girls, Mukuru Kwa Njenga Embakasi, Nairobi.
Kocha wake, Everlyne Onyango anasema ameandaa kikosi hicho tayari kufungua kampeni zao kwa ushindi wa alama tatu na ikiwa mbaya zaidi watoke nguvu sawa wala hawapo tayari kupoteza mchezo huo. 'Kwanza inafahamika sisi ndio mabingwa watetezi na kamwe hatupaswi kupoteza mechi ya ufunguzi,'' anasema. Anaongeza kuwa wachezaji wake wamekuwa wakishiriki mechi za ligi sawa na wapinzani wao ambapo wangali fiti michezoni. Embakasi South itategemea huduma za wachana nyavu shuoavu kama Laventine Lihemo (nahodha), Ashley Nasimiyu, Sharon Tsindoli, Sabrina Noor na Judith Akoth.
Kwenye ratiba ya mechi za Jumamosi hii, Kamongo Ladies itachuana na Wilson Aviators, Mukuru Transformers itamenyana na Mukuru Talents nayo St Josephs Starlets itaumana na Desert Venon.
Kwenye ratiba ya Jumapili tarehe 22 Septemba 2024, Embakasi South Ladies United itarejea dimbani kuchuana na Wilson Aviators. Nayo Desert Venon itagarazana na Mukuru Transformers, Macmillan Queens itatifua vumbi dhidi ya Kamongo Ladies nayo St Josephs Starlets itakutanishwa na Mukuru Talent.
Ngarambe ya mwaka huu inashirikisha timu nane ambazo zimpangwa katika makundi mawili. Kundi A linashirikisha: Embakasi South Ladies United, Kamongo Ladies, Wilson Aviators na Macmillan Queens. Nalo Kundi B linajumuisha: Mukuru Talent, Mukuru Transformers, Desert Venon na St Josephs Starlets. Bingwa wa mwaka huu atatuzwa Sh40,000, nafasi ya pili atapokea Sh25,000, nafasi ya tatu na nne zitatuzwa Sh15,000 na Sh10,000 mtawalia.


