Pumwani Sports, Kariadudu Akili Kichwani Robo Fainali za Koth Biro
- heartmediak4
- Nov 12, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 12 Novemba 2024

PUMWANI Sports Club na Kariadudu FC kila moja inapiga hesabu ya mechi za robo fainali za makala ya 47 kuwania taji la Koth Biro. Pumwani ya kocha, David Maina ambayo ndio mabingwa mtetezi ilijikatia tiketi ya robo fainali ilipoadhibu Kakuma Stars kwa mabao 3-2 kwenye mechi ya raundi ya 16 bora iliyochezwa Jumamosi tarehe 10, Novemba 2024 uwanjani Umeme Ziwani,Nairobi. Nao wanasoka wa Kariadudu walisonga mbele waliponasa ufanisi wa magoli 4-1 dhidi ya Mbotela Kamaliza.
Pumwani Sports ilishusha soka safi na kupata mabao hayo ndani ya kipindi cha kwanza kupitia juhudi zake Hussein Ali aliyepiga kombora mbili naye Ahmed Zaid alifunga bao moja. Kipindi cha pili Kakuma Stars ilirejea dimbani kivingine huku ikilenga kusawazisha lakini bahati haikusimama. Dakika 15 kabla ya mchezo kukamilika Richard Oduor alifunga bao moja huku George Otieno akiongeza la pili dakika tano kabla ya kipenga cha mwisho.

''Tumepania kuendeleza mtindo wa kushinda mechi zetu hadi tutinge fainali tuhakikishe tumehifadhi taji hilo,'' anasema kocha wa Pumwani Sports. Anaongeza wanafahamu mechi zijazo hazitakuwa mteremko lakini hawana hofu kabisa wapo imara kukabili wapinzani wao.
Nayo mabao ya Kariadudu yalipatikana kupitia Welfeey Omondi, Nelson Bwakali, Robert Wabwire na Timothy Odhiambo. Kwenye mechi nyingine, tumaini la Tawuun FC kujikatia tikiti ya robo fainali liligonga ukuta ilipoangukia pua kwa kuchapwa mabao 3-1 na Mathare Combined. Washindi waliteremsha mechi safi na kubeba ufanisi huo kupitia juhudi za wanasoka mahiri akiwamo Peter Wanyonyi, Raphael Mark huku wakifaidi pakubwa kufuatia makosa ya mpinzani wao Ricahrd Wanganga aliyejifunga mara moja. Bao la Tawuun la kufutia machozi lilitupiwa wavuni na Arnold Junior.
Wanachezaji wa vikosi hivyo wamejiunga na wenzao wa Mbuta FC, Kamkunji Falcons na Kiambiu Warriors. Mbuta ilizaba Leads United kwa mabao 2-1, Black Mamba ilidungwa bao 1-0 na Kamkunji Falcons huku Kiambiu Warriors ikibeba magoli 2-0 mbele ya Omena FC.



