top of page
Search

Patshika 6 Ligi Kuu ya Hoki Kupigwa Wikendi Hii

  • heartmediak4
  • Aug 9, 2024
  • 1 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 9 Agosti 2024.





KAMPENI za Ligi Kuu ya magongo ya wanaume na wanawake zinaingia wiki ya pili wikendi hii ambapo mechi sita zimepangwa kuchezwa kwenye viwanja tofauti katika Kaunti ya Nairobi. Timu ya wanaume ya Nairobi Simba na Mashujaa ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha USIU-A kila moja itashiriki mechi mbili. Sawa na vikosi hivyo, vipusa wa USIU-A na DFG Wolverines kila moja itashuka mzigoni kuwania alama sita kutokana na patashika mbili.

Kwanza Nairobi Simba itacheza na USIU-A kisha imenyane na Wazalendo. Kwenye mechi ya pili midume wa USIU-A watakabili Sailors.

Nao vipusa wa DFG Wolverines kwanza wataivaa Sliders kisha watakutanishwa na USIU-A maarufu Spartans. Kabla ya mechi hiyo, warembo wa USIU-A kwanza watapepetana na Amira Sailors.

Wanaume wa Sailors watakuwa mbioni kuwania alama tatu baada ya kuanza vibaya walipozabwa mabao 3-0 na Kenya Police wiki iliyopita. ''Tumepania kujituma kiume angalau kushinda mechi hiyo ambapo lazima tuwe makini zaidi ili tusirejelee makosa ya wiki iliyopita,'' alisema kocha wa Sailors, Timothy Kamar. Aliongeza kuwa mechi za kwanza ligi huwa na changamoto zake kwa kuzingatia huwa hatufahamu jinsi wenzetu wanavyocheza. Sailors inajivunia wachezaji kama Moses Omamo, Jairus Musembi, David Mbugua, Robert Wasike na Richard Abudi.

Nao wanaume wa USIU-A wa kocha, John Kabuu pia walianza vibaya waliponyukwa mabao 3-2 na Western Jaguars.

''Tunalenga kubeba alama sita kutokana na mechi hizo mbili ili kupata moyo wa kujikaza kwenye mechi zijazo,'' alisema kocha wa USIU-A. Alikiri kuwa Western Jaguars ilionyesha mechi nzuri na kuashiria huenda ikashusha ushindani mkali kama msimu uliyopita. USIU-A ina wachezaji shupavu kama Samuel Silong (kipa), Samuel Mboge, Brian Kipkorir, Hillary Otieno na Samuel Masinde.

 
 
bottom of page