Patashika 8 Kupigwa Kundi C Ligi ya Daraja la Pili
- heartmediak4
- Nov 22, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Ijumaa 22, Novemba 2024
PATASHIKA nane zimeratibiwa kuchezwa Jumapili hii (tarehe 24, Novemba 2024) kwenye mfululizo wa kampeni za Kundi C kuwania taji la Ligi ya Taifa Daraja la Pili.
Katika mpango mzima mechi za Kundi C msimu huu zinapigiwa chapuo kushuhudia ushindani wa kufa mtu. Kariobangi Legends Youth na Gikuni United FC kila moja itakuwa katika ardhi ya kiamboni kualika Nyahururu Griffions na Kikuyu Township mtawalia.

Itakuwa mechi ya kwanza ya Kariobangi Legends Youth kushiriki kwenye kipute hicho baada ya kuachana na aliyekuwa kocha mkuu, Osborne Monday. Kariobangi Legends Youth itashiriki mechi hiyo baada ya kupararua Utafiti FC kwa magoli 5-0. Raundi hii itakuwa chini ya naibu kocha, Jeremiah Akhayo anayesema kuwa wameandaa kikosi hicho thabiti kukabili wapinzani wao. ''Baada ya kupiga breki kupisha uchanguzi wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kiwnago cha matawi tumekuwa tukipiga tizi kali kujinolea mechi za ligi,'' anasema kocha wa Kariobangi.

Anaongeza kuwa kama kawaida wanatarajia kujituma kiume kuhakikisha wanadunga mtu kwenye mechi hiyo na kuendeleza mtindo wa kutamba. Timu hii inajivunia kushinda mechi zote mbili ambazo imeshiriki. Kariobangi Legends Youth itatagemea huduma za wachezaji wepesi kama Laurence Otieno (nahodha), Bramwel Kavaya, Dennis Murigi, Victor Kunyili na Fidel Mwanzia kati ya wengine.
Nayo Gikuni United itakuwa chini kocha, Joseph Makumi na Claude Sofa huku ikiwinda kubeba ufanisi wa pointi tatu muhimu. ''Tumepania kutumia ardhi ya nyumbani vizuri angalau kushinda mechi hiyo na kujiongezea alama muhimu,'' anasema kocha wa Gikuni United. Anaongeza kuwa pia wanafahamu wapinzani wao wanalenga kuwavuruga. Gikuni United inajivunia wachezaji hodari kama Geoffrey Kariuki, Abdiaziz Hassan na Ezra Mutai.

Kwenye mfululizo wa ratiba hiyo, vijana wa Tusker Youth watazuru uwanja wa Kari Kikuyu kucheza na Utafiti FC, Tatu City itakuwa nyumbani kukaribisha Shofco FC uwanjani Kamae Referal. Nayo Sunshine itamenyana na Blue Nile, Githurai All Stars itakabili Thika Sporting, Royal Fresh FC itakwaruzana na Embakasi United huku RYSA ikikutanishwa na South C Rangers.


