top of page
Search

Patashika 14 Kupigwa Wikendi hii Ligi ya NERL

  • heartmediak4
  • Jul 12, 2024
  • 2 min read

Updated: Jul 13, 2024

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 12 Julai 2024


MECHI 14 zimepangwa kuchezwa wikendi hii(Jumamosi na Jumapili) kwenye kampeni za Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL). Kariobangi Legends Youth, Tena United, Soweto Allstars, Gunners, Lula FC na Babadogo United kila moja itakuwa mbioni kusaka alama sita muhimu baada ya kushiriki michuano miwili. Jumamosi hii tarehe 13 Julai, Soweto All stars itachuana na Gunners kisha Jumapili tarehe 14 Julai itamenyana na Hakati Sportiff FC.






Nayo Kariobangi Legends Youth itavaana dhidi ya Tena United na Babadogo United Jumamosi na Jumapili mtawalia. Jumamosi hii Lula FC itashuka dimbani kucheza na Babadogo United huku ikipangwa kukutanishwa na UEFA Despanol Jumapili ugani Tumaini Primary.

Jumapili,Gunners ya kocha, Brian Kaka itapepetana na Automech FC huku Tena United ikitifua vumbi dhidi ya Mathare North United.

Kwenye mfululizo wa ratiba hiyo, Jumapili Lucky Summer inayokamata nafasi ya pili itaingia mzigoni kukaribisha Maafande wa Utawala Youth FC ugani Babadogo.



Lucky Summer inategemea huduma za wachezaji shupavu akiwamo Dennis Opiyo, Joel Arika, Victor Otieno na Rijkaard Lwa Otieno kati ya wengine.

Naye kocha wa Kariobangi Legends, Geoffrey Wangalwa anasema wamepania kujituma kwa udi na uvumba kulipiza kisasi baada ya kupoteza pointi tatu kwenye mechi ya mwisho wiki mbili zilizopita. ''Tuna imani tutafanya kweli kwenye mechi zote mbili na kuendelea kujiongezea tumaini la kubeba taji la msimu huu na kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja ya pili msimu ujao,'' anasema kocha huyo. Anaongeza kuwa licha ya kukabili upinzani mkali kutoka kwa wapinzani wao wamepania kushiriki mechi zote kama fainali. Kariobangi Legends Youth inajivunia kushinda wapinzani wao wote kwenye mechi za mkondo wa kwanza ambapo inalenga kurejea kama mwanzo.

Endapo Kariobangi itafanikiwa kushinda mechi hizo itazidi kujiongezea tumaini la kuibuka mabingwa msimu huu. Kariobangi inategemea wachezaji wepesi kama Victor Kinyuli, Bramwel Kasaya, George Karani, Ian Onyango (nahodha), Tom Bonface na Lawrence Otieno Kati ya wengine.



Naye meneja wa Babadogo United, Ben Wanjala anasema wachezaji wapo tayari kukabili wapinzani wao tayari kubeba alama sita muhimu. ''Hatuna hofu dhidi ya wapinzani wetu kwa kuzingatia nasi pia tumejiandaa sawa na wao lengo letu likiwa kutwaa ufanisi wa alama zote,'' anasema.

Katika msimamo wa ngarambe hiyo, Kariobangi Legends Youth ingali kifua mbele kwa alama 67, moja mbele ya Lucky Summer baada ya kushuka dimbani mara 27 na 30 mtawalia. Baada ya Utawala Youth kupiga mechi 31 inafunga tatu bora kwa alama 62. Babadogo United inashikilia nne bora kwa alama 61, sita mbele ya Automech FC baada ya kushiriki mechi 27 na 30 mtawalia.

 
 
bottom of page