Patamu Patashika 2 Zikizalisha Magoli 8 Kipute Cha Koth Biro
- heartmediak4
- Sep 3, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 3 Septemba 2024
MAGOLI nane yamejazwa kimiani kwenye mechi mbili za makala ya 47 kuwania taji la Koth Biro zilizochezwa Jumatatu tarehe 2, Septemba 2024 ugani Umeme Ziwani, Nairobi. Kwenye ratiba hiyo, Black Mamba FC ilitoka nguvu sawa mabao 2-2 na Napoli Comrades huku Mathare Combined ikitoka mabao 2-2 dhidi ya Mbotela Kamaliza.

Black Mamba ilipata mabao hayo kupitia Moses Chris na Abel Reuben huku Vincent Nzomo na John Njoroge wakifungia Napoli Comrades. Nao Muya Michael na Peter Wanyonyi waliibuka shupavu kwa Mathare Combined baada ya kila mmoja kutikisa wavu mara moja.
Mbotela Kamaliza ya kocha, Kelly Ameteshe ilijituma kisabuni na kusawazisha kupitia juhudi zake David Moses na Omondi Leon. ''Napongeza wachezaji wangu kwa kujitahidi kiume licha ya kutoapata tatu muhimu,'' anasema kocha wa Mbotela Kamaliza. Anaongeza kuwa ili kujiweka pazuri kusonga mbele watahitaji kushinda mechi mbili zilizosalia. Kwenye mechi za makala yaliyopita Mbotela Kamaliza ilipambana kufa kupona kabla ya kubanduliwa kwenye nusu fainali. Kocha huyo anatoa wito kwa vijana wake wamakinike zaidi kwenye michuano ijayo.

Kwenye mechi zilizopigwa Jumapili tarehe 1, Septemba 2024, Kingpower FC ilitoka nguvu sawa mabao 2-2 na Kahliweed FC huku Sunshine FC ikizabwa mabao 3-2 na Utawala Blackstars.
Mechi hiyo ilianza kwa Kasi huku Newton Bede akifungia Kahliweed bao la Kwanza dakika ya 18. Dakika ya 38 Kingpower ilisawazisha kupitia Stephen Onyango kabla ya Steve Kajiru kuongeza la pili dakika 32 baadaye. Dakika ya 86 Kahliweed ilipata bao la kusawazisha kupitia juhudi zake Basil Onyango.
Michuano hiyo iliendelea kutifua vumbi ambapo Hillary Mulla, Johnson Kalu na Peter Ochieng wa Utawala Blackstars kila mmoja alitikisa wavu mara moja. Upande wa Sunshine magoli hayo yalipatikana kupitia juhudi zake Andrew Mulwa na Ramketi Richard.

."Licha ya kudondosha alama mbili muhimu ninapongeza vijana wangu kwa kuonyesha soka safi mbele ya wapinzani wetu," anasema kocha wa Kahliweed, Henry Anuri. Anaongeza kuwa lazima washinde mechi zilizosalia ili kufuzu kwa mechi za 16 Bora. Naye kocha wa Kingpower, Jaspher Sikune alikubali yaishe na kuhaidi kupambana kiume kwenye mechi zijazo.
Pumwani Sports ndio mabingwa watetezi pia ilikuwa kati ya timu 22 zilizokuwa zinashiriki michuano ya FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL). Kwenye mechi za makala ya 44 Leads United ilimaliza ya pili iliponyukwa mabao 4-2 na Korongez kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 katika fainali. Kwenye makala ya 45 mshindi alikosekana kufuatia hatua ya wafuasi wa Borussia FC kuzua fujo baada ya kikosi hicho kutoka sare tasa na Leads United katika fainali.


