Omena, Ziwani Allstars Zaanza Vyema Kampeni za Koth Biro Cup
- heartmediak4
- Aug 30, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Ijumaa, 30 Agosti 2024
OMENA FC na Ziwani All Stars kila moja imepata mwanzo mzuri kwenye mechi za makala ya saba kuwania taji la Koth Biro zilizopigwa Alhamisi tarehe 29 Agosti ugani Umeme Ziwani, Nairobi. Omena FC imepepeta Kamkunji Falcons kwa mabao 5-2 huku Ziwani All Stars ikibeba ufanisi wa mabao 2-0 mbele ya Eastleigh Stars.
Omena FC ilitembeza soka safi na kuhakikisha imetia kapuni alama tatu muhimu kwenye ufunguzi wa kampeni zake. Wafungaji wa Omena FC walikuwa Freddy Nyahemba na Alfred Ochieng kila mmoja alitikisa wavu mara mbili huku Alfayo Kweya akitupia kimiani goli moja. Nayo Kamkunji FC ilipata mabao hayo kupitia juhudi zake Ian Abraham na Derrick Hope waliocheka na wavu mara moja kila mmoja.

Nao Benson Oluoch na Victor Otieno kila mmoja alitupia bao moja kimiani na kusaidia Ziwani Allstars kusajili ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Eastleigh Stars ugani humo. ''Kwa mtazamo wangu tulikuwa tushinde mchuano huo tena kwa wingi wa mabao ambapo tayari tumeteleza kwa kutofunga mabao mengi,'' anasema kocha wa Ziwani All Stars. John Otieno. Anaongeza kuwa anafahamu wanatarajia kibarua kizito kwenye mechi mbili zijazo. Anashikilia wapinzani wao sio wa kudharau bali ni vikosi vya kuheshimiwa kwa kuzingatia dimbani huwa vinatetemesha. ''Mechi zijazo tutacheza dhidi ya Pumwani Sports na Kiambiu Warriors wala hatuweza kuwadharau lakini tutahitaji ushindi wa mechi moja ili kujiweka pazuri kusonga mbele,'' akasema.

Naye kocha wa Eastleigh Stars, Omar Ahmed Mohammed anasema ana imani watafuzu kwa mechi za hatua ya 16 bora. ''Licha ya kudondosha alama tatu muhimu nina imani kwenye mechi zijazo wachezaji wangu wawili watakuwa wamepona pia wengine wawili watakuja wote hao nilikosa huduma zao kwenye mechi hiyo,' anasema kocha wa Eastleigh. Anashikilia kuwa wamepania kubeba taji la msimu huu hasa baada ya kubaduliwa katika robo fainali kwenye makala ya mwaka uliyopita.

Pumwani Sports ndio mabingwa watetezi. Pumwani Sports ni kati ya timu 22 ambazo hushiriki michuano ya FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL). Kwenye mechi za makala ya 44 Leads United ilimaliza ya pili iliponyukwa mabao 4-2 na Korongez kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 katika fainali. Kwenye makala ya 45 mshindi alikosekana kufuatia hatua ya wafuasi wa Borussia FC kuzua fujo baada ya kikosi hicho kutoka sare tasa na Leads United


