top of page
Search

Omena FC Yamaliza Kibabe na Kusonga Mbele Ngarambe ya Kothbiro

  • heartmediak4
  • Sep 21, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumamosi, 21 Septemba 2024


OMENA FC imemaliza kibabe mchujo wa Kundi E kwenye kampeni za makala ya 47 kuwania taji la Kothbiro baada ya kulipua Kakuma Stars kwa mabao 2-0 ugani Umeme Ziwani, Nairobi Alhamisi tarehe 19 Septemba 2024. Licha ya matokeo hayo Omena na Kakuma Stars kila moja imejikatia tiketi ya kushiriki mechi za raundi ya 16-Bora kwa kuzoa alama tisa na sita mtawalia. Mechi hiyo ilianza kwa kasi ambapo Kelly Ndululu alifunga bao la kwanza kipindi cha kwanza naye Wachira Njuguna aliongeza bao la pili kipindi cha pili. ''Tunafuraha kuzoa ushindi huo na kumaliza mechi za mchujo bila kushindwa,'' anasema kocha wa Omena, Edward Wanyama.


Anaongeza kuwa wanatarajia kuendeleza ubabe huo kwenye mechi ya 16-Bora hadi katika fainali. Anashikilia kuwa ameandaa vijana wake kushiriki kila mechi kama fainali. Anadokeza kuwa wanalenga kubeba ubingwa wa taji la mwaka huu. Naye kocha wa Kakuma Stars, Jama Abdikadhar iliyokuwa imeshinda mechi zake mbili anasema halikosa wachezaji bora kwa kuzingatia alikuwa anafahamu wamefuzu kwa mechi za raundi ya 16 bora. ''Bila shaka wapinzani wetu watarajie kibarua kigumu kwenye mechi zijazo maana tutarejea kwa nguvu kuonyesha ubabe wetu,'' anasema. Anaongeza kuwa wanataka taji la mwaka huu.



Kwenye mechi nyingine ya kundi hilo, Kamkunji Falcons ilituzwa ushindi wa mezani dhidi ya Macmillan Juniors. Licha ya matokeo hayo timu hizo, Kamkunji Falcons na Macmillan Juniors zilibanduliwa kwenye mashindano ya mwaka huu.

Kwenye mechi ya Kundi H, Mbotela Kamaliza ilisonga mbele baada ya kutuzwa ushindi wa mezani dhidi ya Nyoi FC iliyoingia mitini.

Kwenye mechi zilizochezwa Jumatano, Levy Ochieng alicheka na wavu mara moja na kubeba Mathare Combined kudunga Pangani United bao 1-0. Nayo Kiambiu Warriors ilivuna ushindi wa mezani dhidi ya Eastleigh Stars iliyoingia gizani.

Kwenye mechi za Jumanne, Kundi C, Gikomba All Stars ilicharaza Ruaraka All Stars mabao 2-0, Kundi G Kariadudu FC ilivuna bao 1-0 dhidi ya Sunshine FC, Kundi B, Watch and Learn FC ilitoka bila kufungana na Mbuta




Orodha ya baadhi ya timu ambazo tayari zimefuzu kwa mechi za raundi ya 16-Bora inajumuisha: Kundi A, Leads United na Kahliweed. Kundi B, Watch and Learn na Mbuta FC. Kundi C, Kamkunji FC na Ruaraka Allstars kisha Kundi D, Kayole Select na Black Mamba.

Pumwani Sportiff ndio mabingwa watetezi wa taji hilo. Kwenye mechi za makala ya 44 Leads United ilimaliza ya pili iliponyukwa mabao 4-2 na Korongez kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 katika fainali. Kwenye makala ya 45 mshindi alikosekana pale wafuasi wa Borussia FC walipozua fujo baada ya kikosi hicho kutoka sare tasa na Leads United.

 
 
bottom of page