top of page
Search

Olimpiki: Malkia Strikers Kusaka Angalau Seti Moja Mbele ya Brazil

  • heartmediak4
  • Jul 28, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumapili, 28 Julai 2024




WAREMBO wa Malkia Strikers kesho Jumatatu tarehe 19 Julai, watashuka dimbani kukabili Brazil kwenye mechi za Kundi B katika voliboli ya Michezo ya Olimpiki inayoendelea jijini Paris, Ufaransa.


Vipusa hao wa makocha, Japheth Munala na Jos Barasa watamenyana na wapinzani hao siku mbili baada ya kucheza kirafiki na kupigwa seti 3-0. Malkia walizabwa alama za 25-20, 25-22, 25-12.

''Juzi tulicheza na Brazil japo kirafiki ni timu nzuri ambapo ni kati ya vikosi bora duniani lakini hatuwezi kuiogopa lazima tujitume kwa udi na uvumba,'' alisema nahodha wake, Trizah Atuka. Aliongeza kuwa watakuwa mbioni angalau kwa mara ya kwanza kwenye kipute hicho kuwinda ushindi wa seti moja.

Kundi hilo linajumuisha: Brazil inayoshikilia nafasi ya pili duniani, Poland ya nne pia Japan inayokamata nafasi ya saba. Kwenye viwango hivyo Kenya imetua nafasi ya 20 ikiwa ndio inaongoza barani Afrika.


Kwenye mashindano ya Challenger Cup yaliandaliwa nchini Ufilipino mapema mwezi huu, Malkia Strikers ilinyukwa seti 3-0 na Puerto Rico. Itakumbukwa kwenye kipute hicho makala ya mwaka uliyopita Malkia Strikers ilizabwa seti 3-0 na Colombia. Kwenye mechi za kupimana nguvu jijini Miramas, Ufaransa Malkia ilishinda mara mbili kwa seti 3-0 kila moja mbele ya wenyeji Salon De Provence na Istres Provence.


Malkia Strikers inapigwa jeki na wachezaji wawili ambao hushiriki voliboli ya kulipwa katika mataifa ya bara Ulaya. Nao ni Sharon Chepchumba ambaye huchezea PAOK aliyojiunga nayo akitokea klabu ya Aris Thessaloniki. Mwingine ni Veronica Adhiambo ambaye hupigia Tarsus Belediyespor ya Uturuki.


Hii ni mara ya nne Malkia Strikers wanashiriki Michezo ya Olimpiki baada ya kucheza mwaka 2000 (Sydney, Australia), mwaka 2005 (Athens, Ugiriki) na mwaka 2020 (Tokyo, Japan). Hata hivyo baada ya kushiriki makala ya mwaka 2005 walikosekana kwa miaka 16 ambapo hawakushiriki makala ya mwaka 2008 (Uchina), mwaka 2012 (Uingereza) na 2016 (Brazil).


Kikosi kamili: Agripina Kundu, Sharon Chepchumba, Loice Simiyu, Pamela Adhiambo, Veronica Adhiambo, Juliana Namutira, Leonida Kasaya, Trizah Atuka (nahodha) na naibu wake Edith Wisa. Wengine Emmaculate Nekesa, Belinda Barasa, Lorine Chebet na Esther Mutinda.

Maofisa: Makocha Japheth Munala na Josp Barasa, kocha wa kupiga tizi, Janet Wanja na Mududa Waweru (meneja).

 
 
bottom of page