Olimpiki: Malkia Strikers Kufungua Kampeni Zake Dhidi ya Brazil
- heartmediak4
- Jul 27, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumamosi, 27 Julai 2024.

VIPUSA wa timu ya voliboli maarufu Malkia Strikers wamepangwa kukabili Brazil kwenye ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki inayoanza leo jijini Paris Ufaransa. Malkia Strikers ya kocha, Japheth Munala ambayo imepangwa Kundi B itacheza dhidi ya mabingwa watetezi hao mnamo (Julai 29) wiki ijayo. Kisha itaingia ukumbini tena kucheza mechi ya pili (Julai 31) mbele ya Poland kabla ya kumenyana na Japan (Agosti 3).
Wanadada hao wanatazamiwa kupata ushindani mkali kwa kuzingatia wapinzani wao wote wamepangwa katika nafasi bora kwenye msimamo wa viwango vya mchezo huo duniani (FIVB). Brazil inashikilia nafasi ya pili, Poland ya nne nayo Japan inakamata nafasi ya saba. Kwenye viwango hivyo Kenya imetua nafasi ya 20 ikiwa ndio inaongoza barani Afrika.
Kwenye mashindano ya Challenger Cup yaliandaliwa nchini Ufilipimo mapema mwezi huu, Malkia Strikers ilipigwa seti 3-0 na Puerto Rico. Itakumbukwa kwenye kipute hicho makala ya mwaka uliyopita Malkia Strikers ilinyukwa seti 3-0 na Colombia. Kwenye mechi za kupimana nguvu jijini Miramas, Ufaransa Malkia ilishinda mara mbili kwa seti 3-0 kila moja mbele ya
Salon De Provence na Istres Provence.
''Kwanza tunashukuru wafadhili wetu ikiwemo serikali kupitia kamati ya Michezo ya Olimpiki ya Kenya (NOCK), Mozzartbet, Java House kati ya wengine kwa kutushika mkono kwenye maandalizi yetu,'' alisema naibu nahodha, Edith Wisa. Aliongeza kuwa wapo tayari kujituma kisabuni kwenye mechi za makala ya mwaka huu. Malkia Strikers imeshiriki ngarambe hiyo mara tatu wala haijawahi kushinda seti hata moja.
Kwa kuzingatia inatarajia mtihani mgumu mbele ya wapinzani wao itakuwa mbioni kusaka angalau ushindi wa seti moja. Kwenye makala ya mwisho mwaka 2020 yaliyoandaliwa jijini Tokyo Japan, Malkia ilimaliza mwisho nafasi ya 12.
Kikosi kamili: Agripina Kundu, Sharon Chepchumba, Loice Simiyu, Pamela Adhiambo, Veronica Adhiambo, Juliana Namutira, Leonida Kasaya, Trizah Atuka (nahodha) na naibu wake Edith Wisa. Wengine Emmaculate Nekesa, Belinda Barasa, Lorine Chebet na Esther Mutinda.
Maofisa: Makocha Japheth Munala na Josp Barasa, kocha wa kupiga tizi, Janet Wanja na Mududa Waweru(meneja).


