top of page
Search

Nzau: Tumezingua Wenyewe Mbele ya Kariobangi Legends

  • heartmediak4
  • Nov 12, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumanne, 12 Novemba 2024


TIMU ya Dandora Legends imeona giza baada ya kubamizwa kwa mabao 2-1 na Kariobangi Legends Wazee kwenye mchuano wa kirafiki uliochezwa Jumapili tarehe 10, Novemba uwanjani Kariobangi Primary, Nairobi. Dandora Legends iliteremsha mechi safi mbele ya wenyeji wao na kuonyesha sio ya kupuuza.

Wachezaji hao wakiongozwa na nahodha, Moses Nzau walionekana kuwazidi nguvu wenyeji wao ndani ya kipindi cha kwanza. .

Dandora Legends ilitangulia kupata bao hilo la pekee kipindi cha kwanza kupitia Kevin 'Ragos' Mwangale. Kwa jumla bao hilo lilichochea mechi hiyo ambapo pande zote zilianza kushusha mashambulizi kibao kuwinda ushindi.






Kariobangi iliendelea kuonyesha soka la kushirikiana vyema dimbani ikiwinda mabao ambapo ilisawazisha kupitia Fidel Mwanzia. Kariobangi iliyokuwa chini ya kocha, Kelvin 'Odengo' Otieno iliendelea kusaka bao la ushindi na kufanikiwa kutimiza azma hiyo kupitia juhudi zake Idris Amadi. ''Nilikuwa kocha wa mechi hiyo na nilipata wakati mgumu maana wachezaji wengi walikuwa wanataka kuingia uwanjani lakini tatizo nililikuwa kuamua nani angetoka,'' kocha wa Kariobangi anasema. Anaongeza kuwa licha ya wapinzani wao kutangulia kufunga hatimaye kikosi chake kilifanya kweli na kuzoa alama zote muhimu. Anashikilia kuwa wachezaji wake wanazidi kupata motisha kwa jinsi wanavyozidi kushinda mechi zao.




Anadokeza kuwa ufanisi huo unaashiria kwamba timu hiyo ipo imara kuendelea kufanya vizuri kwenye mechi za kupimana nguvu. ''Tuliangukia pua mbele ya wenyeji wetu lakini pia wao walifahamu haikuwa mteremko kiukweli tuliwazidia nguvu mchezoni lakini walitumia vyema nafasi mbili walizopata kiufupi tulizingua wenyewe,'' anasema nahodha wa Dandora Legends. Aliongeza kuwa wanapanga mechi ya marudiano ambapo watakaribisha Kariobangi katika uwanja wa Dandora Stadium. Kariobangi Legends imeibuka moto wa kuotea mbali kwenye mechi za kirafiki katika Kaunti ya Nairobi. Kwenye mechi zingine za hivi karibuni Kariobangi ilikandamiza Githurai 45 Wazee kwa magoli 5-1 kisha kuagana mabao 3-3 dhidi ya Baba Dogo Legends.

 
 
bottom of page