top of page
Search

sammy Kempes Kutoa Maokoto ya Washindi wa Koth Biro

  • heartmediak4
  • Nov 12, 2024
  • 2 min read


Na HEART MEDIA

Jumanne, 12 Novemba 2024


MWANIAJI wa kiti cha Rais wa Shirikisho la Soka ya Kenya (FKF), Sammy 'Kempes' Owino ametangaza kwamba atatoa Sh190,000 kutuza washindi wa shindano la makala ya 47 kuwania taji la Koth Biro.



Ofisa mkuu wa ngarambe hiyo, Issa Barugote amethibitisha hayo na kushukuru mwaniaji huyo kwa kuwapiga jeki kwa ufadhili huo. ''Kwa niaba ya kamati ya kipute cha mwaka huu nashukuru Kempes amekuja wakati mwafaka,'' anasema ofisa huyo.


Anaongeza kuwa ujio wa mwaniaji huyo umesaidia pakubwa kwa kuzingatia alipiga milundi huku na kule akisaka ufadhili bila mafanikio. Mshindi atatuzwa Sh100,000, nafasi ya pili atapokea Sh50,000 huku timu zitakaomaliza nafasi ya tatu na nne zikipongezwa kwa Sh30,000 na Sh10,000 mtawalia.

Kando na fedha hizo mwaniaji huyo atagharamia marupurupu ya waamuzi wa mechi zilizosalia (rono fainali, nusu fainali na fainali), pia marupurupu ya maafisa wa polisi watakaotoa usalama kwenye mechi zilizosalia.


Kuhusu mechi za raundi ya 16 bora, wachezaji wa Kahliweed FC walizua fujo

dakika tano kabla ya kipengo cha mwisho wakiwa wamefungwa mabao 3-0 na Watch and Learn FC kwenye patashika iliyopigiwa ugani Umeme Ziwani, Nairobi Jumatatu tarehe, 11 Novemba 2024.



Licha ya Kahliweed kuonekana kulemea wapinzani wao kipindi cha kwanza kilikamilika sare tasa. Kipindi cha pili, Watch and Learn FC ya kocha, Bonface Omino ilirejea dimbani kivingine na kuashiria ilipania kubeba ushindi. Abubakar Ali alifungia Watch and Learn FC bao la kwanza dakika ya 47. Dakika kumi baadaye Rodgers Okoth alitupia kimiani bao la pili huku Stanley Isoye akifunga bao la tatu dakika tano kabla ya kipengo cha mwisho wakati mechi ilipotibuka vijana wa Kahliweed walipovamia msaidizi wa mwamuzi wa mechi hiyo.


''Bila shaka ninapongeza wachezaji wangu kwa kujituma na kuhakikisha wametwaa tikiti ya robo fainali,'' alisema kocha wa Watch and Learn FC. Aliongeza kuwa wamepania kuendeleza mtindo wa kufanya kweli kwenye mechi zilizosalia.

Kwenye mechi za makundi, Watch and Learn FC ilisonga mbele ilipomaliza kileleni mwa Kundi B kwa alama saba, mbili mbele ya Mbuta FC. Nayo Kahliweed iliyokuwa imepangwa Kundi A iliibuka ya pili kwa alama tano huku Leads United ikiwa kifua mbele kwa alama sita.

 
 
bottom of page