Nyati FC, Gateway FC Zajitosa 16 Bora Kipute Cha Ruben FM Cup.
- heartmediak4
- Sep 3, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 3 Septemba 2024
TIMU ya Nyati FC na Gateway FC kila moja imezoa alama tatu na kutinga 16 bora kwenye mechi za makala ya saba kuwania taji la Ruben FM Cup. Nyati FC ya kocha, Michael Wanjohi ilipepeta Minto FC kwa mabao 2-1 kwenye mechi zilizochezwa Jumapili, 1 Septemba 2024 ugani Vision, Mukuru Kwa Njenga Embakasi, Nairobi.

Nayo Gateway FC ambayo imepangwa Kundi B ilizoa ushindi wa mezani baada ya wapinzani wao Homeboys kuingia mitini. Nyati ambayo imepangwa Kundi F, ilishusha soka safi na kulemea wapinzani wao kupitia mabao ya Rodgers Mbasu na Brian Mukosi. Naye Jingiri Jingiri alifungia Minto bao la kufuatia machozi.
''Bila shaka vijana wangu walijituma kiume maana walikuwa lazima washinde ili tusonge mbele,'' anasema mwanzilishi wa Nyati, Curtis Saiti. Anapongeza wachana nyavu wake kwa kupiga hatua na kuwataka kuwa makini zaidi kwenye mechi zijazo. Anadokeza kuwa mechi zijazo zitakuwa za muondoano ambapo wakiteleza tu watakuta mwana sio wao.
Kwenye matokeo hayo, Amusha FC ilitoka nguvu sawa mabao 2-2 na Deportivo FC. Mabao ya Amusha yalitupiwa kimiani na Lawrence Abok nao Suleiman Anyande na Geoffrey Anjera walifungia Deportivo. Kwenye msimamo wa Kundi F, Nyati FC inaongoza kwa alama 7, mbili mbele ya Amusha FC.

Kwenye mechi za Kundi D, Real Warriors ilizoa tiketi ya 16 bora ilipokanganya Busec FC kwa magoli 3-2. Kelvin Kioko wa Real Warriors alipiga kombora mbili huku Kelvin Aziz akifunga goli moja. Nao James Maina na Francis Sammy walifungia Busec bao moja kila mmoja.
Embakasi East FC ambayo imepangwa Kundi H imeondokea licha ya kuvuna ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Barca Veterans pia iliyobanduliwa kutoka ngarambe ya mwaka huu. Mukuru Wazee FC ilitoka sare tasa na Tala All Stars, huku NAS FC na Simba FC kila moja zikiachana nguvu sawa goli 1-1 dhidi ya Corinthians na United Kings. Bao la NAS lilitupiwa wavuni na Frank Fadhili huku Alex Mutinda akitingia Corinthians. Nao Sabarstiane Mashedi na Ismail Abdi walifungia Simba na United Kings mtawalia.

Nao Michael Mutisya na Sebastian Marwa kila mmoja alitikisa wavu mara moja na kusaidia Milan FC kutoka nguvu sawa mabao 2-2 dhidi ya Green Santos. Wafungaji wa Green Santos walikuwa Vincent Muli na David Wanjla. Kwenye msimamo wa Kundi G, ingawa Meteorite FC ina mechi moja kapuni tayari imefuzu kwa 16 bora baada ya kufikisha alama sita, tatu mbele ya Dream Team kutokana na mechi mbili kila moja. NAS ambayo imepangwa Kundi H imefuzu baada ya kuibuka kifua mbele kwa alama saba, mbili mbele ya Corinthians FC.


