Nyati FC, Corinthians FC Kila Moja Ange Kubeba Ruben FM Cup
- heartmediak4
- Aug 13, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Jumanne, 13 Agosti 2024
NYATI FC na Corinthians FC ni kati ya vikosi ambavyo vimefungua vyema kampeni za soka kufukuzia taji la makala ya saba la Ruben FM Cup.
Nyati FC ambayo hutiwa makali na kocha, Michael Wanjohi iliadhibu Deportivo Leon FC kwa mabao 2-0 kwenye patashika zilizochezwa wikendi ugani Vision Mukuru Kwa Njenga, Embakasi Nairobi.
Nao wachana nyavu wa Barca Veteran waliona giza walipozimwa kwa mabao 2-1 na Corinthians ugani Embakasi Girls. Nyati ilitembeza soka safi na kufanikiwa kuzoa mabao hayo kupitia juhudi zake Kelly Otieno na Shadrack Kamata. ''Bila shaka tulianza kampeni zetu kwa kishindo hali inayotutia motisha zaidi kupambana kwa udi na uvumba kwenye mechi zilizosalia za makundi,'' anasema kocha wa Nyati FC. Anaongeza kuwa mwaka huu wamepania kushusha soka la kibiashara ili kuhakikisha wameibuka mabingwa. Anashikilia kwamba wachezaji wake wanatosha mboga kunyamazisha wapinzani wao.

Nao Morris Musau na Fredrick Achola kila mmoja alifungia Corinthians bao moja huku Taiwo Hassan akisawazishia Barca Veteran. ''Ninapongeza vijana wangu kwa kuzoa alama tatu muhimu katika utangulizi lakini nawahimiza wawe makini zaidi hasa kuzuia kutofungwa kwenye mechi zijazo mradi tujiweka pazuri vitani,'' anasema kocha wa Corinthians,Silas Kivasu. Anashikilia kwamba wanafahamu wapinzani wao wamejipanga kiume kuonyesha uwezo wao huku wakitumia michuano hiyo kunoa makali yao.

Kwenye matokeo hayo, Amusha FC ilitoka nguvu sawa mabao 2-2 na Minto FC, naye Ooko Vincent alitikisa wavu mara moja na kubeba NAS kudunga Embakasi East FC bao 1-0. Muhanji Vishal alipiga kombora moja lililotosha mboga kusaidia Green Santos kuzaba Homeboys bao 1-0. Nao Felix Kyalo na Remy Ouma kila mmoja alitikisa wavu mara moja na kubeba Real Warriors na Dream Team kuzaba United Kings na AFC Embakasi Branch bao 1-0 kila moja mtawalia.
Mshindi wa makala ya mwaka huu kitengo cha wanaume atatuzwa Sh100,000 huku bingwa wa kina dada akitia kibindoni Sh40,000. Kwa wanaume nafasi ya pili na tatu watapokea Sh70,000 na 40,000 huku nambari nne akipongezwa kwa Sh20,000. Kwa wanawake timu itakayoibuka ya pili itazoa Sh25,000 nafasi ya tatu na nne zitatuzwa Sh15,000 na Sh10,000 mtawalia. Kwa tuzo za kibinafsi, mfungaji bora, mnyakaji bora, mchezaji mwenye nidhamu na kocha bora kwa wanaume na wanawake kila mmoja atapokea Sh5000.


