top of page
Search

Nyahururu Griffons Hoi Mbele Ya Kariobangi Legends Youth Daraja 2

  • heartmediak4
  • Nov 25, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumatatu 25, Novemba 2024



NYAHURURU Griffons imerejea makwao mikono mitupu baada ya kufinywa na Kariobangi Legends Youth kwenye mechi ya Kundi C kuwania taji la Ligi ya Taifa Daraja la Pili. Kariobangi Legends Youth ya kocha, Jeremiah Akhayo ilibeba ushindi wa mabao 3-0 kwenye patashika iliyochezwa Jumapili tarehe 24, Novemba 2024 uwanjani Our Lady of Fatuma, Kariobangi North, Nairobi.


Ni ushindi wa tatu kwa vijana wa Kariobangi Legends Youth wanaoshiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza. Kocha wake anasema vijana wake walipiga tizi ya wiki moja wala hawakuonyesha soka waliotarajia kwenye mchuano huo. Licha ya hayo wachana nyavu hao walishusha soka safi na kuhakikisha wamezoa alama tatu muhimu katika ardhi ya nyumbani.



Ushirikiano mwema dimbani ulichangia vijana hao kupata bao la kwanza kunako dakika ya tano kupitia juhudi zake Siraji 'Konde' Abdallah. Pande zote ziliendelea kuwinda mabao bila mafanikio huku wenyeji Kariobangi Legends Youth wakizidi kuonyesha soka la hali ya juu kuliko wageni wao. Dakika 23 baadaye Kariobangi Legends Youth ilionyesha kwamba ingali na kiu cha kufunga mabao zaidi ambapo Paul Odhiambo aliongeza goli la pili. Kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza wenyeji walikuwa kifua mbele kwa mabao 2-0.



Katika kipindi cha pili, Siraji 'Konde' Abdallah aliongeza bao la tatu dakika ya 68. ''Vijana wangu walifanya kazi ya kupendeza licha ya kupitia changamoto kiasi za kimaisha,'' anasema kocha wake.

Anaongeza wanatazamia kuendeleza mtindo huo kwenye mechi zijazo. Naye mwenyekiti wa klabu hiyo, Eric Otieno Atanga anapongeza wachezaji wake kwa kujituma kwa udi na uvumba na kuhakikisha wamezoa ushindi wa pointi tatu muhimu kwenye mechi hiyo. Anadokeza kuwa ana imani wachezaji wake watazidi kuimarisha mchezo wao kwenye mechi zijazo.


Nayo RYSA ilikubali kulala kwa kudungwa bao 1-0 na South C Rangers, Kikuyu Township ilitwaa ufanisi wa mabao 2-1 mbele ya Gikuni United, Githurai All Stars (GAS) ilipigwa mabao 3-2 na Thika Sporting, Utafiti iliagana nguvu sawa mabao 2-2 dhidi ya Tusker Youth. Mabao ya Tusker yalipatikana kupitia Calvin Odhiambo na Kevin Ochieng. Royal Fresh na Tatu City kila moja ilitoka sare tasa mbele ya Embakasi United na Shofco FC mtawalia. Naye John 'Sancho' Thuku alitkisa wavu mara mbili na kubeba Aspire Nyahururu kuzoa mabao 2-1 mbele ya Balaji FC kwenye mechi za Kundi D kipute hicho.

 
 
bottom of page