Ngarambe ya Ruben FM Cup Kukunjua Jamvi Wikendi Hii
- heartmediak4
- Aug 9, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Ijumaa, 9 Agosti 2024

MICHUANO ya Makala ya saba kuwania taji la Ruben FM Cup imeratibiwa kung'oa nanga rasmi wikendi hii kwenye viwanja vya Vision na Embakasi Girls, eneo la Embakasi Nairobi. Jumamosi hii tarehe 10 Agosti, ugani Vision, kwenye mechi za Kundi F, Nyati FC itateremka dimbani kukabili Deportivo Leon FC. Nayo Embakasi East FC ambayo imepangwa Kundi H itatifua vumbi dhidi ya NAS FC.
Ugani Embakasi Girls, kwenye mechi za Kundi H, Corinthians FC itakabili Barca Veterans, Kundi B, Homeboyz itavaana na Green Santos. ''Tumepania kujituma kiume ili kuanza kampeni zetu vizuri kwa kuzoa alama tatu muhimu,'' anasema mlenzi wa Nyati FC, Curtis Saiti. Anashikilia kuwa lazima wapambane kufa kupona mwaka huu kwa kuzingatia wanataka kufanya vyema kuliko makala yaliyopita. Nyati FC ya kocha, Michael Wanjohi itategemea wachezaji kama Elvis Omolet, Elvis Mboya, Kelvin Okech, Felix Ochieng, Jesse Inanga na Rodgers Tangasi.
''Msimu huu tumepania kujituma kwa udi na uvumba tuhakikishe tunafanya vizuri ambapo kwenye utangulizi wetu maana tunalenga kubeba pointi tatu muhimu,'' anasema kocha wa Corinthians, Silas Kivasu. Anaongeza kuwa wanafahamu wapinzani wao wamejipanga kuwalipua. Corinthians inategemea wachana nyavu kama Alex Mutinda (nahodha), Brian Iwobi, Denis 'Lefty', Aron Kimanzi, John Andere na Analo Steven kati ya wengine.

Katika ratiba ya Jumapili tarehe 11 Agosti, ugani Vision Kelvin 'Ras' Vallery ataongoza City Foxes kukabili Rising City nayo AFC Leopards Embakasi South itacheza na Dream Team. United Kings itamenyana na Real Warriors huku Amusha FC ikikutanishwa na Minto FC. ''Tutakuwa makini zaidi kusudi tushinde mechi ya utangulizi maana tunafahamu wapinzani nao pia wamejipanda kiume,'' anasema kocha wa City Foxes. Anaongeza kuwa wamepania kupambana mwanzo mwisho wahakikishe wanazima wapinzani wao. Timu hiyo itategemea huduma za wanasoka kama Joseph 'Sita' Wambua, Peter 'Nzagi' Majanga, Joseph 'Sancho' Mutungi, Leonard 'Letfy' Poriot na Apollo 'Totoo' Mbugua.
Mshindi wa makala ya mwaka huu kitengo cha wanaume atatuzwa Sh100,000 huku bingwa wa kina dada akitia kibindoni Sh40,000. Kwa wanaume nafasi ya pili na tatu watapokea Sh70,000 na 40,000 huku nambari nne akipongezwa kwa Sh20,000. Kwa wanawake timu itakayoibuka ya pili itazoa Sh25,000 nafasi ya tatu na nne zitatuzwa Sh15,000 na Sh10,000 mtawalia. Kwa tuzo za kibinafsi, mfungaji bora, mnyakaji bora, mchezaji mwenye nidhamu na kocha bora kwa wanaume na wanawake kila mmoja atapokea Sh5000.



