top of page
Search

Ngarambe ya Koth Biro Kuingia Raundi ya 3 Wikendi hii

  • heartmediak4
  • Sep 13, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Ijumaa, 13 Septemba 2024



MECHI za makala ya 47 kuwania taji la Koth Biro zimeratibiwa kuingia raundi ya tatu wikendi hii ugani Umeme, Ziwani Nairobi. Jumamosi hii tarehe 14, Septemba mechi mbili zitagaragazwa ugani humo ambapo kwenye Kundi A, Kingpower FC itaumana na Mlango FC, Kundi B Ajax Rock City itakabili Shauri Moyo Sportiff. Jumapili tarehe15, Septemba, Leads United itashuka dimbani kuchuana na Kahliweed FC.

Kwenye mechi moja iliyochezwa Alhamisi tarehe 12, Septemba, Kakuma Stars ilinyorosha Macmillan Juniors kwa mabao 3-2. Mabao ya Kakuma Stars yalipatikana kupitia Richard Oduor aliyepiga kombora mbili naye Salim Dolio alitupia kimiani bao moja.



Jumatano tarehe 11, Septemba, Nyoi FC ilikung'utwa mabao 6-2 na Mathare Combined nayo Pangani FC ilitoka bila kufungana dhidi ya Mbotela Kamaliza. Mechi za Jumanne tarehe 10, Septemba, Sunshine ilicharaza Taawun FC kwa mabao 2-0 nayo Utawala Blackstars ililala kwa mabao 2-1 mikononi mwa Kariadudu FC.


Mlango ya kocha, James Mwangi itahitaji kunyamazisha Kingpower endapo imepania kunasa tiketi ya raundi ya 16 bora. Mlango inavuta mkia kwa alama moja baada ya kutoka nguvu sawa mechi moja na kupoteza mchuano mmoja.

''Tunafahamu lazima tujitume kwa udi na uvumba tuhakikishe tunashinda mechi hiyo ili tufikishe alama nne na kujiweka pazuri kusonga mbele,'' anasema kocha huyo. Hata hivyo Mlango ikishinda mechi hiyo pia itahitaji kuomba Mola Kahliweed FC ilitoka nguvu sawa ama iadhibiwe na Leads United. Endapo Kingpower itaibuka mshindi itafikisha pointi nne na kujiongezea tumaini la kusonga mbele.



Nayo Ajax Rock City ya kocha, Joseph Morte itakuwa na kibarua kigumu maana ni lazima ishinde wapinzani wao ili kujiweka pazuri kunasa tiketi ya kusonga mbele. Ajax inashikilia nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi hilo kwa alama moja baada ya kutoka nguvu sawa na kuagana bila kufungana. ''Kwanza tutahitaji kushinda mechi hiyo tena kwa idadi ya mabao mengi kwa kuzingatia tutafikisha alama nne sawa na Mbuta FC,'' anasema kocha wa Ajax Rock City. Anaongeza kuwa kampeni za msimu huu zimeshuhudia ushindani mkali kinyume na matarajio yao.

Leads United ya kocha, issa Winston tayari imefuzu kushiriki mechi za raundi ya 16 bora kwani katika msimamo wa Kundi A kamwe hakuna mpinzani anaweza kuipiku. Leads inaongoza kundi hilo kwa alama sita baada ya kushinda mechi mbili ambazo imeshiriki ambapo hata ikipoteza dhidi ya Kahliweed bado itasalia kileleni. ''Licha ya kwamba tufuzu kwa raundi ya 16 bora hatuna lingine tutakuwa tunahitaji ushindi wa alama tatu ili kumaliza mechi zetu kibabe,'' anasema kocha huyo. Anaongeza kwamba bado hawana la ziada kwani wamepania kupambana kiume kuhakikisha wanabeba taji la msimu huu.


Kwenye mechi za makala yaliyotangulia Leads United ilimaliza ya pili iliponyukwa mabao 4-2 na Korongez kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1 katika fainali. Kwenye ngarambe ya mwaka 2021 mshindi alikosekana kufuatia hatua ya wafuasi wa Borussia FC kuzua fujo baada ya kikosi hicho kutoka sare tasa na Leads United. Shindano hilo ni kati ya michuano ambayo hushirikisha wachezaji wa klabu za ligi tofauti hapa nchini.

 
 
bottom of page