NERL: Lucky Summer, Kariobangi L. Youth Zinashusha Soka la Kibiashara
- heartmediak4
- Jul 18, 2024
- 2 min read
Na HEART MEDIA
Alhamisi, 18 Julai 2024

KOCHA Dan Nguya wa Lucky Summer anakiri kuwa wana kibarua kigumu kwenye mechi za FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL) muhula huu. Anasema kuwa licha ya kukabili ushindani mkali wamepania kupambana kiume kupigania tiketi ya kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja ya Pili msimu ujao. Anadokeza hayo licha ya kutoka bao 1-1 dhidi ya Utawala Youth wikendi.
Lucky Summer ilipata bao hilo kupitia Rijkaard Lwa Otieno. Naye Clinton Kisiavuki alifungia Utawala Youth ambayo hutiwa makali na kocha Bill Oporia. ''Kusema ukweli tunapambana kufa mtu lakini nyakati zingine tunaangukia pua na kudondosha alama muhimu,'' alisema. Aliongeza kuwa aste aste watawapiku wapinzani wao.

Lucky Summer ilizoa alama moja huku Kariobangi Legends Youth ya kocha, Geoffrey Wangalwa ikishinda mechi mbili kwa bao 1-0 kila moja dhidi ya Tena United na Babadogo United. Bramuel Kavaya na Dennis Wafula walifungia Kariobangi kwenye mechi ya Tena United na Babadogo United mtawalia.
''Licha ya kupata mtihani mgumu hatujayeyusha tumaini la kumaliza kileleni na kunasa tiketi ya kupandishwa ngazi msimu ujao,'' alisema kocha wa Kariobangi.
Aliongeza kuwa wamepania kunyamazisha wapinzani wao kwenye mechi zijazo.
Analaumu vijana wake kwa kupoteza alama 14 muhimu kwenye mechi sita walipotoka nguvu sawa mara nne na kudondosha patashika mbili.
Licha ya Babadogo kupigwa na Kariobangi Legends Youth kwenye mechi ya pili ilizoa ushindi mnono wa mabao 4-1 mbele ya Lula FC. Mabao ya Babadogo yalipatikana kupitia Simon Barasa, Justus Odhiambo, George Mukavana na Winston Mang'oli.

'Hakuna kuvumua tunapiga soka kibiashara kuwania tiketi ya kusonga mbele maana tunaamini tunaweza pia tumekaa pazuri kujituma na kuwapiku wapinzani wetu,'' alisema meneja wa Babadogo, Ben Wanjala. Aliongeza wanashiriki kila mechi kama fainali ambapo wakizidi kuzoa matunda mema na wenzao walitelezea bila shaka watatua kileleni.
Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Tumaini FC inayoendelea kupigania kujinasua kutoka mduara wa kushushwa ngazi ilipigwa mabao 2-1 na Fortune Kinderen. Francis Mang'ele alifungia Tumaini FC bao la kufuta machozi.
Naye kocha, Josiah Olang aliongoza Automech FC kuadhibu Gunners kwa mabao 3-2 kupitia Peter Wambua, George Omondi na Musa Kombo. Stephen Ajode wa Automech FC aliibuka mchezaji bora kwenye mechi hiyo baada ya kutoa pasi ya mabao hayo.

''Hatujakaa vibaya tunazidi kukaz buti kwenye kampeni zetu kufukuzia tiketi ya kupanda ngazi,'' alisema kocha wa Automech. Gunners ilipokezwa kichapo cha pili ilipolala kwa mabao 3-1 mbele ya Soweto Allstars, Santos Hotspurs ilinyukwa magoli 3-1 na Wendani Allstars. Nayo Ruai United ilikanyanga Gor Mahia Youth kwa mabao 2-1, Tena United ilibeba mabao 2-0 mbele ya Mathare North United, Rada Sports ilibamiza Umoja Rhino kwa mabao 2-1 huku Lula FC ikiagana sare tasa dhidi ya UEFA Despanol.
Kariobangi Legends Youth ingali kifua mbele kwa kuzoa alama 73, sita mbele ya Lucky Summers baada ya kuingia mzigoni mara 29 na 31 mtawalia. Babadogo United inashikilia tatu bora kwa alama 64, moja mbele ya Utawala Youth.


