top of page
Search

NERL: Lucky Summer Imeketi Mkao wa Subira Ikitegea Tiketi ya Daraja la Pili

  • heartmediak4
  • Aug 27, 2024
  • 2 min read

Na HEART MEDIA

Jumanne, 27 Agosti 2024


LUCKY Summer imeibuka ya pili kwenye mechi za FKF Kundi B Ligi ya Kanda ya Nairobi Mashariki (NERL) licha ya kutoka nguvu bao 1-1 na Mathare North Youth kwenye patashika ya Jumapili tarehe 25 Agosti. Ingawa ina mechi moja kapuni inashikilia nafasi ya pili kwa alama 93 ambapo hata wapinzani wao Utawala Youth wakishinda mechi yao hawawezi kuwapiku.






Ni wazi kuwa Lucky Summer ya kocha, Dan Nguya imejiweka pazuri kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja ya Pili endapo nafasi itapatikana. ''Bila shaka ninapongeza vijana wangu kwa kazi nzuri waliofanya licha ya kutotimiza azma yetu kubeba taji la muhula huu,'' anasema kocha wa Lucky Summer. Anaongeza kuwa wana imani watashinda mechi ya mwisho dhidi ya Gunners itakayochezwa Jumamosi ijayo tarehe 31 Agosti. Anaongeza kwamba kamwe hawana hofu wanaamini watapata nafasi ya kushiriki ligi ya hadhi ya juu msimu ujao.



Kwenye matokeo ya michuano ya Jumapili, Tena United ilipepeta Rada Sports kwa magoli 5-1. Wafungaji wa Tena United walikuwa Fanuel Chibole aliyecheka na wavu mara nne naye Benard Otieno alitupia kimiani bao moja.


Nayo Kariobangi Legends Youth inayotarajia kutawazwa mabingwa wa kipute hicho ilibeba mabao 3-0 mbele ya Wendani Allstars. Kariobangi ya kocha, Geoffrey Wangalwa na Jeremiah Akhayo ilipata ushindi huo kupitia juhudi zake Brian Idelia, Bramwel Kavaya na Dennis Wafula waliotikisa wavu mara moja kila mmoja. ''Kama kawaida tunapongeza wechezaji wetu kwa kuendelea kuonyesha ubabe wao licha ya kwamba tayari tumebeba taji,'' anasema kocha huyo. Anaongeza kuwa wamepitia changamoto nyingi lakini hatimaye wametimiza azma yao kuibuka mabingwa sasa wanasubiri kupandishwa daraja muhula ujao.


Kwenye mfululizo huo, Kelly Ndululu alitikisa wavu mara mbili nao Chris Orengo na Allan Mwangi kila mmoja alifunga bao moja na kubeba Automech FC kuzaba Lula FC Mabao 4-1. Santos Hotspurs ilipigwa mabao 3-1 na Soweto Allstars, Gor Mahia Youth ilisajili mabao 3-1 mbele ya Hakati Sportiff, Gunners iliangusha Umoja Rhinos kwa mabao 2-1 huku Babadogo United ikiadhibiwa kwa mabao 4-2 na Pumwani Sports. Fortune Kinderen ilicharazwa mabao 6-0 na Utawala Youth nayo Tumaini FC ilitoka sare tasa dhidi ya Ruai United.

 
 
bottom of page